2 Kings 23:5-11
5 aAkawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. 6 bAkaiondoa nguzo ya Ashera kutoka kwenye Hekalu la Bwana, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wa kawaida. 7 cAkabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada za miungu, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana na mahali wanawake walipofuma kwa ajili ya Ashera.8 dYosia akawaleta makuhani wote wa Bwana kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji. 9 eIngawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu hawakuhudumu katika madhabahu ya Bwana katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu miongoni mwa ndugu zao.
10 fKisha mfalme akanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe au binti yake katika moto kwa mungu Moleki. 11 gAkaondoa kutoka kwenye ingilio la Hekalu la Bwana wale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathan-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa jua.
Copyright information for
SwhNEN