Deuteronomy 15:1-11

Mwaka Wa Kufuta Madeni

(Walawi 25:1-7)

1 aKila mwisho wa miaka saba ni lazima mfute madeni. 2Hivi ndivyo itakavyofanyika: Kila mkopeshaji atafuta mkopo aliomkopesha Mwisraeli mwenzake. Hatamtaka Mwisraeli mwenzake au ndugu yake amlipe hilo deni, kwa sababu wakati wa Bwana wa kufuta madeni umetangazwa. 3 bUnaweza kudai malipo kwa mgeni, lakini lazima ufute kila deni ambalo unamdai ndugu yako. 4 cHata hivyo, hapatakuwepo maskini miongoni mwenu, kwa kuwa katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kuimiliki kama urithi wenu, atawabariki sana, 5 dikiwa tutamtii Bwana Mungu wenu kikamilifu na kuwa waangalifu kuyafuata maagizo haya yote ninayowapa leo. 6 eKwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki kama alivyoahidi, nanyi mtawakopesha mataifa mengi lakini hamtakopa kwa yeyote. Mtatawala mataifa mengi lakini hakuna taifa litakalowatawala ninyi.

7 fIkiwa kuna mtu maskini miongoni mwa ndugu zenu, katika mji wowote wa hiyo nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, msiwe na moyo mgumu wala usimfumbie mkono ndugu yako aliye maskini. 8 gAfadhali fungua mikono yako na umkopeshe kwa hiari chochote anachohitaji. 9 hJihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi. 10 iMpe kwa ukarimu na ufanye hivyo bila kinyongo moyoni, ndipo kwa sababu ya hili Bwana Mungu wenu atakubariki katika kazi zako zote na kwa kila kitu utakachokiwekea mkono wako. 11 jSiku zote watakuwepo watu maskini katika nchi. Kwa hiyo ninawaamuru mwe na mikono iliyokunjuliwa kuwaelekea ndugu zenu, kuwaelekea maskini na wahitaji katika nchi yenu.

Copyright information for SwhNEN