Isaiah 34:5-15


5 aUpanga wangu umekunywa na kushiba huko mbinguni,
tazama, unashuka katika hukumu juu ya Edomu,
wale watu ambao nimeshawahukumu,
kuwaangamiza kabisa.
6 bUpanga wa Bwana umeoga katika damu,
umefunikwa na mafuta ya nyama:
damu ya kondoo na mbuzi,
mafuta kutoka figo za kondoo dume.
Kwa maana Bwana ana dhabihu huko Bosra,
na machinjo makuu huko Edomu.
7 cNyati wataanguka pamoja nao,
ndama waume na mafahali wakubwa.
Nchi yao italowana kwa damu,
nayo mavumbi yataloa mafuta ya nyama.

8 dKwa sababu Bwana anayo siku ya kulipiza kisasi,
mwaka wa malipo,
siku ya kushindania shauri la Sayuni.
9 eVijito vya Edomu vitageuka kuwa lami,
mavumbi yake yatakuwa kiberiti kiunguzacho,
nchi yake itakuwa lami iwakayo!
10 fHaitazimishwa usiku wala mchana,
moshi wake utapaa juu milele.
Kutoka kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa,
hakuna mtu yeyote atakayepita huko tena.
11 gBundi wa jangwani na bundi mwenye sauti nyembamba wataimiliki,
bundi wakubwa na kunguru wataweka viota humo.
Mungu atanyoosha juu ya Edomu
kamba ya kupimia ya machafuko matupu,
na timazi ya ukiwa.
12 hWatu wake wa kuheshimiwa hawatakuwa na chochote
kitakachoitwa ufalme huko,
nao wakuu wao wote watatoweka.
13 iMiiba itaenea katika ngome za ndani,
viwawi na michongoma itaota
kwenye ngome zake.
Itakuwa maskani ya mbweha,
makao ya bundi.
14 jViumbe vya jangwani vitakutana na fisi,
nao mbuzi-mwitu watalia wakiitana;
huko viumbe vya usiku vitastarehe pia
na kujitafutia mahali pa kupumzika.
15 kBundi wataweka viota huko na kutaga mayai,
atayaangua na kutunza makinda yake
chini ya uvuli wa mabawa yake;
pia huko vipanga watakusanyika,
kila mmoja na mwenzi wake.
Copyright information for SwhNEN