Isaiah 44:9-20


9 aWote wachongao sanamu ni ubatili,
navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.
Wale ambao wanazitetea ni vipofu,
ni wajinga, nao waaibika.
10 bNi nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,
ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?
11 cYeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,
mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.
Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,
watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.

12 dMuhunzi huchukua kifaa
na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto,
hutengeneza sanamu kwa nyundo,
huifanyiza kwa nguvu za mkono wake.
Huona njaa na kupoteza nguvu zake,
asipokunywa maji huzimia.
13 eSeremala hupima kwa kutumia kamba
na huuchora mstari kwa kalamu;
huchonga kwa patasi
na kutia alama kwa bikari.
Huifanyiza katika umbo la binadamu,
la mwanadamu katika utukufu wake wote,
ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu.
14 fHukata miti ya mierezi,
huchukua mtiriza au mwaloni.
Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni,
au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.
15 gNi kuni ya binadamu:
yeye huchukua baadhi yake na kuota moto,
huwasha moto na kuoka mkate.
Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu,
huitengeneza sanamu na kuisujudia.
16 hSehemu ya kuni huziweka motoni,
akapikia chakula chake,
hubanika nyama na kula hadi ashibe.
Huota moto na kusema,
“Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”
17 iMabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake;
yeye huisujudia na kuiabudu.
Huiomba na kusema,
“Niokoe; wewe ni mungu wangu.”
18 jHawajui chochote, hawaelewi chochote,
macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona,
akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.
19 kHakuna anayefikiri,
hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema,
“Sehemu yake nilitumia kwa kuni;
hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake,
nikabanika nyama na kuila.
Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki?
Je, nisujudie gogo la mti?”
20 lHujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha;
hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema,
“Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?”
Copyright information for SwhNEN