Isaiah 53:4-11


4 aHakika alichukua udhaifu wetu
na akajitwika huzuni zetu,
hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,
akapigwa sana naye, na kuteswa.
5 bLakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,
alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;
adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,
na kwa majeraha yake sisi tumepona.
6 cSisi sote, kama kondoo, tumepotea,
kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,
naye Bwana aliweka juu yake
maovu yetu sisi sote.

7 dAlionewa na kuteswa,
hata hivyo hakufungua kinywa chake;
aliongozwa kama mwana-kondoo
apelekwaye machinjoni,
kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,
hivyo hakufungua kinywa chake.
8 eKwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.
Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?
Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,
alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.
9 fWakamfanyia kaburi pamoja na waovu,
pamoja na matajiri katika kifo chake,
ingawa hakutenda jeuri,
wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

10 gLakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana
kumchubua na kumsababisha ateseke.
Ingawa Bwana amefanya maisha yake
kuwa sadaka ya hatia,
ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,
nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.
11 hBaada ya maumivu ya nafsi yake,
ataona nuru ya uzima na kuridhika;
kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki
atawafanya wengi kuwa wenye haki,
naye atayachukua maovu yao.
Copyright information for SwhNEN