John 19:17-27
17 aYesu, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha). 18 bHapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wengine wawili, mmoja kila upande wake, naye Yesu katikati.19 cPilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Yesu, likasema: “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi.” 20 dKwa kuwa mahali hapo Yesu aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini. 21 eViongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.”
22Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”
Mavazi Ya Yesu Yagawanywa
23 fAskari walipokwisha kumsulubisha Yesu, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono bali limefumwa tangu juu hadi chini. 24 gWakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.”Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema,
“Wanagawana nguo zangu,
na vazi langu wanalipigia kura.”
Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.
25 hWakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene. 26 iYesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” 27 jkisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake.
Copyright information for
SwhNEN