Lamentations 4:4-21


4 aKwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga
umegandamana na kaakaa la kinywa chake,
watoto huomba mkate,
lakini hakuna yeyote awapaye.

5 bWale waliokula vyakula vya kifahari
ni maskini barabarani.
Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau
sasa wanalalia majivu.

6 cAdhabu ya watu wangu
ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,
ambayo ilipinduliwa ghafula
bila kuwepo mkono wa msaada.

7Wakuu wao walikuwa wamengʼaa kuliko theluji
na weupe kuliko maziwa,
miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,
kuonekana kwao kama yakuti samawi.

8 dLakini sasa ni weusi kuliko masizi;
hawatambulikani barabarani.
Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,
imekuwa mikavu kama fimbo.

9 eWale waliouawa kwa upanga ni bora
kuliko wale wanaokufa njaa;
wanateseka kwa njaa, wanatokomea
kwa kukosa chakula kutoka shambani.

10 fKwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma
wanapika watoto wao wenyewe,
waliokuwa chakula chao
watu wangu walipoangamizwa.

11 g Bwana ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;
ameimwaga hasira yake kali.
Amewasha moto katika Sayuni
ambao umeteketeza misingi yake.

12 hWafalme wa dunia hawakuamini,
wala mtu yeyote wa duniani,
kwamba adui na watesi wangeweza kuingia
kwenye malango ya Yerusalemu.

13 iLakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,
na maovu ya makuhani wake,
waliomwaga ndani yake
damu ya wenye haki.

14 jSasa wanapapasa papasa barabarani
kama watu ambao ni vipofu.
Wamenajisiwa kabisa kwa damu,
hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.

15 kWatu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!
Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”
Wanapokimbia na kutangatanga huku na huko,
watu miongoni mwa mataifa wanasema,
“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”

16 l Bwana mwenyewe amewatawanya;
hawaangalii tena.
Makuhani hawaonyeshwi heshima,
wazee hawakubaliki.

17 mZaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,
kwa kutazamia bure msaada;
tuliangalia kutoka minara yetu
kwa taifa lisiloweza kutuokoa.

18 nWatu walituvizia katika kila hatua
hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu.
Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,
kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.

19 oWaliotufuatia walikuwa wepesi
kuliko tai angani;
walitusaka juu milimani
na kutuvizia jangwani.

20 pMpakwa mafuta wa Bwana, pumzi ya uhai wetu hasa,
alinaswa katika mitego yao.
Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake
tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.

21 qShangilia na ufurahi, ee Binti Edomu,
wewe unayeishi nchi ya Usi.
Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,
Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.
Copyright information for SwhNEN