Leviticus 11:24-40

Wanyama Ambao Ni Najisi

24 a“ ‘Mtajinajisi kwa wanyama hawa. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 25 bYeyote atakayebeba mizoga ya viumbe hawa ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

26“ ‘Kila mnyama mwenye ukwato ulioachana lakini haukugawanyika kabisa, au yule asiyecheua, huyo ni najisi kwenu; yeyote agusaye mzoga wowote wa hao atakuwa najisi. 27Miongoni mwa wanyama wote watembeao kwa miguu minne, wale watembeao kwa vitanga vyao ni najisi kwenu; yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 28 cYeyote atakayebeba mizoga yao ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Wanyama hawa ni najisi kwenu.

29“ ‘Kuhusu wanyama watambaao juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu: kicheche, panya, aina yoyote ya mijusi mikubwa, 30 dguruguru, kenge, mijusi ya ukutani, goromoe na kinyonga. 31Hao wote watambaao juu ya ardhi ni najisi kwenu. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 32 eIkiwa mmoja wao atakufa na kuangukia juu ya kitu fulani, chombo hicho, hata kikiwa cha matumizi gani, kitakuwa najisi, kiwe kimetengenezwa kwa mti, nguo, ngozi au gunia. Kiweke ndani ya maji; kitakuwa najisi mpaka jioni, kisha kitakuwa safi tena. 33 fIkiwa mmoja wa wanyama aliyekufa ataangukia ndani ya chungu, kila kilichomo katika chungu hicho kitakuwa najisi, nawe ni lazima uvunje chungu hicho. 34Chakula chochote ambacho chaweza kuliwa lakini kikawa kimeingia maji kutoka kwenye chungu hicho ni najisi, na kitu chochote cha majimaji ambacho chaweza kunyweka kutoka kwenye chungu hicho ni najisi. 35Chochote ambacho mzoga wa mmojawapo utaangukia kitakuwa najisi. Jiko au chungu cha kupikia ni lazima kivunjwe. Ni najisi, nawe ni lazima uvihesabu kuwa najisi. 36Lakini chemchemi au kisima, mahali pa kuchota maji, patakuwa safi, lakini yeyote atakayegusa moja ya mizoga hii ni najisi. 37Kama mzoga ukianguka juu ya mbegu zozote ambazo ni za kupanda, zinabaki safi. 38Lakini kama mbegu imetiwa maji na mzoga ukaanguka juu yake, hiyo mbegu ni najisi kwenu.

39 g“ ‘Kama mnyama ambaye mnaruhusiwa kumla akifa, yeyote atakayeugusa mzoga wake atakuwa najisi mpaka jioni. 40 hYeyote atakayekula sehemu ya mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Yeyote atakayebeba mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

Copyright information for SwhNEN