Luke 23:26-43

Kusulubiwa Kwa Yesu

(Mathayo 27:32-44; Marko 15:21-32; Yohana 19:17-27)

26 aWalipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Yesu. 27 bIdadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. 28 cYesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29 dKwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ 30 eNdipo

“ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!”
na vilima, “Tufunikeni!” ’
31 f Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”

32 gWatu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Yesu ili wakasulubiwe. 33Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. 34 hYesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

35 iWatu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.”

36 jAskari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, 37 kna wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”

38 lKwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.

Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.

39 mMmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Kristo? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”

40Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu iyo hiyo? 41 nSisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”

42 oKisha akasema, “Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”

43 pYesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Paradiso maana yake bustani nzuri, hapa ina maana mahali zinapokwenda roho za wacha Mungu, yaani watakatifu.


Copyright information for SwhNEN