Mark 5:1-20
Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo
(Mathayo 8:28-34; Luka 8:26-39)
1 aWakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika nchi ya Wagerasi. 2 bYesu alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini akakutana naye. 3Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo. 4Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. 5Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.6Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake. 7 cAkapiga kelele kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” 8Kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”
9Yesu akamuuliza, “Jina lako ni nani?”
Akamjibu, “Jina langu ni Legioni, ▼
▼Legioni maana yake ni Jeshi.
kwa kuwa tuko wengi.” 10Akamsihi Yesu sana asiwapeleke nje ya nchi ile. 11Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima. 12Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.” 13Basi Yesu akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao 2,000, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.
14Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakatoka kwenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia. 15 eWalipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu legioni akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa. 16Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia. 17 fBasi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika nchi yao.
18 gYesu alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Yesu waende pamoja. 19 hYesu hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokuhurumia.” 20 iYule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Yesu aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.
Copyright information for
SwhNEN