Matthew 17:14-23
Yesu Amponya Kijana Mwenye Pepo
(Marko 9:14-29; Luka 9:37-43)
14 aWalipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15 b“Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”17 cYesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.
19 dKisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”
20 eAkawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [ 21Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]”
22 fSiku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. 23 gNao watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika sana.
Copyright information for
SwhNEN