c Mwa 47:11; Kut 20:12; Law 19:3; Kum 5:16; Mit 10:1; 23:24; Mt 19:19; Yn 19:25-27; Efe 6:2; 1Tim 5:4
1 Samuel 22
Daudi Akiwa Adulamu Na Mispa
1 aDaudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. 2 bWale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao 400 walikuwa pamoja naye.3 cKutoka huko Daudi akaenda Mispa huko Moabu na kumwambia mfalme wa Moabu, “Naomba uwaruhusu baba yangu na mama yangu waje kukaa nawe mpaka nijue nini Mungu atakachonifanyia.” 4 dHivyo akawaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu, nao wakakaa naye muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni.
5 eNdipo nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae ngomeni. Nenda katika nchi ya Yuda.” Hivyo Daudi akaondoka na kwenda katika msitu wa Herethi.
Sauli Awaua Makuhani Wa Nobu
6 fBasi Sauli akasikia kwamba Daudi na watu wake wameonekana. Sauli akiwa na mkuki mkononi, alikuwa ameketi chini ya mti wa mkwaju kwenye kilima huko Gibea, maafisa wake wote wakiwa wamesimama kumzunguka. 7 gSauli akawaambia, “Sikilizeni enyi watu wa Benyamini! Je, mwana wa Yese atawapa ninyi nyote mashamba na mashamba ya mizabibu? Je, atawafanya ninyi nyote majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia? 8 hJe, ndiyo sababu ninyi mkapanga hila mbaya dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu ambaye ameniambia ni lini mwanangu alifanya agano na mwana wa Yese. Hapana hata mmoja wenu anayejishughulisha nami wala anayeniambia kwamba mwanangu amechochea mtumishi wangu kunivizia, kama afanyavyo leo.”9 iLakini Doegi Mwedomu, ambaye alikuwa akisimama na maafisa wa Sauli, akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija kwa Ahimeleki mwana wa Ahitubu huko Nobu. 10 jAhimeleki akamuuliza Bwana kwa ajili yake; pia akampa vyakula na ule upanga wa Goliathi Mfilisti.”
11Kisha mfalme akatuma watu wamwite kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, waliokuwa makuhani huko Nobu, nao wote wakaja kwa mfalme. 12Sauli akasema, “Sikiliza sasa, mwana wa Ahitubu.”
Akajibu, “Naam, bwana wangu.”
13Sauli akamwambia, “Kwa nini umepanga shauri baya dhidi yangu, wewe na mwana wa Yese, ukampa vyakula na upanga, tena hukumuuliza Mungu kwa ajili yake, na kwa sababu hiyo ameasi dhidi yangu na kunivizia, kama afanyavyo leo?”
14 kAhimeleki akamjibu mfalme, “Ni nani miongoni mwa watumishi wako wote aliye mwaminifu kama Daudi, mkwewe mfalme, kiongozi wa walinzi wako na anayeheshimika sana katika watu wa nyumbani mwako? 15Je, siku hiyo ilikuwa ndiyo ya kwanza kumwomba Mungu kwa ajili yake? La hasha! Mfalme na usiwashutumu watumishi wako wala yeyote wa jamaa ya baba yake, kwa kuwa mtumishi wako hafahamu lolote kabisa kuhusu jambo hili lote.”
16 lLakini mfalme akasema, “Ahimeleki, hakika utakufa, wewe na jamaa yote ya baba yako.”
17 mNdipo mfalme akawaamuru walinzi wake waliokuwa kando yake: “Geukeni na kuwaua makuhani wa Bwana, kwa sababu nao pia wamejiunga na Daudi. Walijua kuwa alikuwa anakimbia, wala hawakuniambia.”
Lakini maafisa wa mfalme hawakuwa radhi kuinua mkono kuwaua makuhani wa Bwana.
18 nKisha mfalme akamwagiza Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Hivyo basi Doegi Mwedomu, akageuka na kuwaua. Siku ile aliwaua watu themanini na watano wavaao visibau vya kitani. 19 oPia akaupiga Nobu kwa upanga, mji wa makuhani, wakiwemo wanaume na wanawake, watoto wadogo na wale wanyonyao, ngʼombe wake, punda na kondoo.
20 pLakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi. 21Akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa Bwana. 22 qKisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile, wakati Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli. Mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa ya baba yako yote. 23 rKaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.”
Copyright information for
SwhNEN