2 Kings 22
Yosia Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 34; 35:20-27)
1 aYosia alikuwa na miaka minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na mmoja. Mama yake aliitwa Yedida binti Adaya, kutoka Boskathi. 2 bAkafanya yaliyo mema machoni pa Bwana na kuenenda katika njia zote za Daudi baba yake. Hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.3 cKatika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, Mfalme Yosia akamtuma mwandishi Shafani mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, kwenda katika Hekalu la Bwana. Akasema: 4 d“Panda uende kwa Hilkia, kuhani mkuu, umwambie ahesabu zile fedha ambazo zimeletwa katika Hekalu la Bwana, ambazo mabawabu wamekusanya kutoka kwa watu. 5 eWaambie waikabidhi kwa watu walioteuliwa kusimamia kazi ya Hekalu. Waamuru watu hawa wawalipe wafanyakazi ambao wanakarabati Hekalu la Bwana: 6 fwale maseremala, wajenzi na waashi. Waambie pia wanunue mbao na mawe yaliyochongwa ili kukarabati Hekalu. 7 gLakini hawahitajiki kutoa hesabu ya fedha walizokabidhiwa, kwa sababu wanafanya kwa uaminifu.”
8 hHilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Sheria ndani ya Hekalu la Bwana.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma. 9Kisha Shafani mwandishi akamwendea mfalme na kumpa taarifa akisema: “Maafisa wako wametoa ile fedha ambayo ilikuwa ndani ya Hekalu la Bwana na imekabidhiwa mikononi mwa wasimamizi wa marekebisho ya Hekalu.” 10 iNdipo Shafani mwandishi akampasha mfalme habari kwamba: “Hilkia kuhani amenipa kitabu hiki.” Naye Shafani akakisoma kile kitabu mbele ya mfalme.
11Mfalme aliposikia maneno ya kile Kitabu cha Sheria, akararua mavazi yake. 12 jAkatoa maagizo haya kwa Hilkia kuhani, Ahikamu mwana wa Shafani, Akbori mwana wa Mikaya, Shafani mwandishi, na Asaya mtumishi wa mfalme: 13 k“Nendeni mkamuulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu na Yuda wote kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Bwana ni kubwa inayowaka dhidi yetu kwa sababu baba zetu hawakuyatii maneno ya kitabu hiki. Hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa humo kutuhusu sisi.”
14 lHilkia kuhani, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya wakaenda kuongea na nabii mke Hulda, ambaye alikuwa mke wa Shalumu mwana wa Tikwa, mwana wa Harhasi mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu katika Mtaa wa Pili.
15Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, 16 m‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, kulingana na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho mfalme wa Yuda alichosoma. 17 nKwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine, na kunighadhibisha kwa sanamu zote zilizotengenezwa kwa mikono yao, hasira yangu itawaka dhidi ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’ 18 oMwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Bwana, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia: 19 pKwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Bwana uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Bwana. 20 qKwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ”
Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.
Copyright information for
SwhNEN