2 Kings 8:7-15
Hazaeli Anamuua Ben-Hadadi
7 aElisha akaenda Dameski, naye Ben-Hadadi mfalme wa Aramu alikuwa mgonjwa. Mfalme alipoambiwa, “Mtu wa Mungu ametoka mbali akapanda hadi hapa,” 8 bmfalme akamwambia Hazaeli. “Chukua zawadi na uende kumlaki huyo mtu wa Mungu. Muulize Bwana kupitia yeye, kwamba, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”9Hazaeli akaenda kumlaki Elisha, akiwa amechukua zawadi ya kila kitu kizuri kilichopatikana Dameski, mizigo iliyobebwa na ngamia arobaini. Akaingia ndani na kusimama mbele yake, akasema, “Mwanao Ben-Hadadi mfalme wa Aramu amenituma niulize, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”
10Elisha akajibu, “Nenda ukamwambie, ‘Hakika utapona’; lakini Bwana amenifunulia kwamba kweli atakufa.” 11 cElisha akamkazia Hazaeli macho kwa nguvu mpaka akaona aibu. Kisha mtu wa Mungu akaanza kulia.
12 dHazaeli akauliza “Kwa nini bwana wangu analia?”
Elisha akajibu, “Kwa sababu najua mabaya utakayowatendea Waisraeli. Utachoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, kuwatupa chini kwa nguvu watoto wachanga, na kuwatumbua wanawake wenye mimba.”
13 eHazaeli akasema, “Itawezekanaje mtumishi wako, aliye mbwa tu, kufanya tendo la ajabu namna hiyo?”
Elisha akamjibu, “Bwana amenionyesha kuwa utakuwa mfalme wa Aramu.”
14Kisha Hazaeli akamwacha Elisha na kumrudia bwana wake. Ben-Hadadi akamuuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akajibu, “Aliniambia kwamba hakika utapona.” 15 fLakini kesho yake Hazaeli akachukua nguo nzito, akailoweka ndani ya maji, akaitandaza juu ya uso wa mfalme, hivyo akafa. Kisha Hazaeli akaingia mahali pake kuwa mfalme wa Aramu.
Copyright information for
SwhNEN