2 Samuel 3
1 aVita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi.2 bWana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni:
Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli;
3 cmzaliwa wake wa pili alikuwa Danieli ▼
▼Jina lingine lake ni Kileabu.
mwana wa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli;wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri;
4 ewa nne, Adoniya mwana wa Hagithi;
wa tano, Shefatia mwana wa Abitali;
5wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi.
Hawa ndio waliozaliwa kwa Daudi huko Hebroni.
Abneri Anamwendea Daudi
6 fWakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli. 7 gBasi Sauli alikuwa amekuwa na suria, jina lake Rispa binti wa Aiya. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?”8 hAbneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke! 9 iMungu na amshughulikie Abneri, tena kwa ukali, ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kile Bwana alichomwahidi kwa kiapo, 10 jna kuuhamisha ufalme kutoka kwenye nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba.” 11Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri.
12Ndipo Abneri akatuma wajumbe kwa niaba yake kwa Daudi, kumwambia, “Nchi hii ni ya nani? Fanya mapatano na mimi, nami nitakusaidia kuiweka Israeli yote juu yako.”
13 kDaudi akasema, “Vyema, nitafanya mapatano nawe. Lakini nahitaji jambo moja kwako: Usije mbele yangu mpaka umemleta Mikali binti Sauli wakati utakapokuja kuniona.” 14 lKisha Daudi akapeleka wajumbe kwa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, kudai, “Nipe Mikali mke wangu, ambaye nilimposa mwenyewe kwa mahari ya magovi 100 ya Wafilisti.”
15 mKwa hiyo Ish-Boshethi akatoa amri kwamba Mikali achukuliwe kutoka kwa Paltieli mumewe, mwana wa Laishi. 16 nHata hivyo, mumewe alikwenda pamoja naye, akilia nyuma ya mkewe njia yote hadi Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani!” Kwa hiyo akarudi.
17 oAbneri akafanya shauri pamoja na wazee wa Israeli, akasema, “Muda mrefu mmetaka kumfanya Daudi mfalme wenu. 18 pSasa fanyeni hivyo! Kwa maana Bwana alimwahidi Daudi akisema, ‘Kwa kupitia Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka mikononi mwa Wafilisti na kutoka mikononi mwa adui zako wote.’ ”
19 qPia Abneri mwenyewe akazungumza na kabila la Benyamini. Kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kila kitu ambacho Israeli na nyumba yote ya Benyamini walichotaka kufanya. 20 rWakati Abneri aliyekuwa na watu ishirini pamoja naye, alipokuja kwa Daudi huko Hebroni, Daudi akamwandalia karamu pamoja na watu wake. 21 sNdipo Abneri akamwambia Daudi, “Niache niende mara moja nikakusanye Israeli yote kwa ajili ya mfalme bwana wangu, ili waweze kufanya mapatano na wewe, ili kwamba uweze kutawala juu ya yote yale ambayo moyo wako unaonea shauku.” Basi Daudi akamuaga Abneri, naye akaenda kwa amani.
Yoabu Amuua Abneri
22Wakati huo huo, watu wa Daudi na Yoabu walirudi kutoka kwenye kushambulia, nao wakarudi na nyara nyingi mno. Lakini Abneri hakuwa tena pamoja na Daudi huko Hebroni, kwa sababu Daudi alikuwa amemruhusu aende zake, naye akaenda kwa amani. 23Yoabu na askari wote aliokuwa nao walipowasili, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri alikuwa amekuja kwa mfalme na kwamba mfalme alikuwa amemruhusu aende zake, na kwamba alikwisha ondoka kwa amani.24Basi Yoabu alikwenda kwa mfalme na kumwambia, “Ni nini hiki ulichofanya? Tazama, Abneri alikuja kwako. Kwa nini ukamwacha aende? Sasa amekwenda! 25 tWajua Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya na kuchunguza nyendo zako na kupata kila kitu unachokifanya.”
26Ndipo Yoabu akamwacha Daudi na kutuma wajumbe wamfuate Abneri, nao wakamrudisha kutoka kisima cha Sira. Lakini Daudi hakufahamu jambo hili. 27 uBasi Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando ndani ya lango, kama vile kuzungumza naye faraghani. Ili kulipiza kisasi damu ya nduguye Asaheli, Yoabu akamchoma mkuki tumboni palepale, naye akafa.
28 vBaadaye, Daudi aliposikia kuhusu jambo hili, akasema, “Mimi na ufalme wangu kamwe hatuna hatia mbele za Bwana kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri. 29 wDamu yake na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na juu ya nyumba yote ya baba yake! Kamwe asikosekane yeyote katika nyumba ya Yoabu mwenye kidonda chenye usaha, au ukoma au mwenye kuegemea fimbo au aangukaye kwa upanga au kupungukiwa na chakula.”
30 x(Yoabu na Abishai ndugu yake walimuua Abneri kwa sababu alikuwa amemuua Asaheli ndugu yao katika vita huko Gibeoni.)
31 yKisha Daudi akamwambia Yoabu na watu wote aliokuwa pamoja nao, “Rarueni nguo zenu na mvae nguo za gunia na mtembee mkiomboleza mbele ya Abneri.” Mfalme Daudi mwenyewe akatembea nyuma ya jeneza. 32 zWakamzika Abneri huko Hebroni, naye mfalme akalia kwa sauti kwenye kaburi la Abneri. Pia watu wote wakalia.
33 aaMfalme akaimba ombolezo hili kwa ajili ya Abneri:
“Je, ilipasa Abneri afe kama afavyo mpumbavu?
34 abMikono yako haikufungwa,
miguu yako haikufungwa pingu.
Ulianguka kama yeye aangukaye
mbele ya watu waovu.”
Nao watu wote wakamlilia tena.
35 acKisha watu wote wakaja kumsihi Daudi ale chochote kulipokuwa kungali bado mchana; lakini Daudi akaapa, akisema, “Mungu na anishughulikie, tena kwa ukali, kama nikionja mkate au kitu kingine chochote kabla ya jua kutua!”
36Watu wote wakaona hilo nao ikawapendeza; naam, kila kitu mfalme alichofanya kiliwapendeza. 37Kwa hiyo siku ile watu wote na Israeli yote wakajua kwamba mfalme hakushiriki katika mauaji ya Abneri mwana wa Neri.
38 adKisha mfalme akawaambia watu wake, “Je, hamfahamu kwamba mkuu na mtu mashuhuri ameanguka katika Israeli leo? 39 aeNami leo ingawa ni mfalme mpakwa mafuta, mimi ni dhaifu, nao hawa wana wa Seruya wananizidi nguvu. Bwana na amlipize mtenda maovu sawasawa na matendo yake maovu!”
Copyright information for
SwhNEN