Ephesians 5
Kuenenda Nuruni
1 aKwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, 2 bmkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.3 cLakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu. 4 dWala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu. 5 eKwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu. 6 fMtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii. 7Kwa hiyo, msishirikiane nao.
8 gKwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru 9 h(kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli), 10 inanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana. 11 jMsishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. 12 kKwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini. 13 lLakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana, 14 mkwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana:
“Amka, wewe uliyelala,
ufufuke kutoka kwa wafu,
naye Kristo atakuangazia.”
15Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 nmkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 oKwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana. 18 pPia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. 19 qMsemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, 20 rsiku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
21 sNyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.
Mafundisho Kuhusu Wake Na Waume
22 tNinyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana. 23 uKwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake. 24 vBasi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.25 wNinyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake 26 xkusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, 27 yapate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia. 28Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. 29Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Kristo anavyolitunza Kanisa lake. 30 zSisi tu viungo vya mwili wake. 31 aa“Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.” 32Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Kristo na Kanisa. 33Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.
Copyright information for
SwhNEN