Esther 3
Hila Ya Hamani Kuwaangamiza Wayahudi
1 aBaada ya matukio haya, Mfalme Ahasuero alimheshimu Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, akampandisha na kumpa kiti chake cha heshima cha juu sana kuliko wakuu wengine wote. 2 bMaafisa wote wa mfalme waliokaa langoni mwa mfalme walipiga magoti na kumpa Hamani heshima, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru hili kuhusu Hamani. Lakini Mordekai hakumpigia magoti wala kumheshimu.3Kisha maafisa wa mfalme waliokuwa langoni mwa mfalme walimuuliza Mordekai, “Kwa nini hutii agizo la mfalme?” 4 cSiku baada ya siku walizungumza naye lakini hakukubali. Kwa hiyo walimweleza Hamani kuona kama tabia ya Mordekai itaweza kuvumiliwa, kwa maana alikuwa amewaambia kuwa yeye ni Myahudi.
5Wakati Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima alighadhibika. 6 dHata hivyo baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumuua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani, Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahasuero.
7 eKatika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.
8 fKisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa. 9Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta 10,000 ▼
▼Talanta 10,000 za fedha ni sawa na tani 340.
za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.” 10Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kwenye kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui wa Wayahudi. 11Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”
12 hKisha siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza waandishi wa mfalme waliitwa. Wakaandika barua kwa kila jimbo na katika kila lugha ya watu kama agizo la Hamani lilivyotoka kwa mfalme, kwa watawala wa majimbo mbalimbali, na wakuu wa watu mbalimbali. Hizi ziliandikwa kwa jina la Mfalme Ahasuero mwenyewe na kutiwa muhuri wa pete yake mwenyewe. 13 iBarua zilipelekwa na tarishi katika majimbo yote ya mfalme zikiwa na amri ya kuharibu, kuua na kuangamiza Wayahudi wote, wadogo kwa wakubwa, wanawake na watoto wadogo, siku moja, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, na pia kuteka nyara vitu vyao. 14Nakala ya andiko la amri ilipaswa kutolewa kama sheria katika kila jimbo, na kufahamishwa kwa watu wa kila taifa ili waweze kuwa tayari kwa siku ile.
15 jKwa kuharakishwa na amri ya mfalme, matarishi walikwenda na andiko lilitolewa katika mji wa ngome ya Shushani. Mfalme na Hamani waliketi na kunywa, lakini mji wa Shushani ulifadhaika.
Copyright information for
SwhNEN