Ezekiel 13
Manabii Wa Uongo Walaumiwa
1Neno la Bwana likanijia kusema: 2 a“Mwanadamu, tabiri dhidi ya manabii wa Israeli wanaotabiri sasa. Waambie hao ambao hutabiri kutokana na mawazo yao wenyewe: ‘Sikia neno la Bwana! 3 bHili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ole wao manabii wapumbavu wafuatao roho yao wenyewe na wala hawajaona chochote! 4 cManabii wako, ee Israeli, ni kama mbweha katikati ya magofu. 5 dHamjakwea kwenda kuziba mahali palipobomoka katika ukuta ili kuukarabati kwa ajili ya nyumba ya Israeli, ili kwamba isimame imara kwenye vita katika siku ya Bwana. 6 eMaono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Bwana amesema,” wakati Bwana hakuwatuma, bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. 7 fJe, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu hapo msemapo, “Bwana asema,” lakini Mimi sijasema?8 g“ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ya uongo wa maneno yenu na kwa madanganyo ya maono yenu, Mimi ni kinyume na ninyi, asema Bwana Mwenyezi. 9 hMkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuandikwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.
10 i“ ‘Kwa sababu ni kweli wanapotosha watu wangu, wakisema, “Amani,” wakati ambapo hakuna amani, pia kwa sababu, wakati ukuta dhaifu unapojengwa, wanaufunika kwa kupaka chokaa, 11 jkwa hiyo waambie hao wanaoupaka chokaa isiyokorogwa vyema kwamba ukuta huo utaanguka. Mvua kubwa ya mafuriko itanyesha, nami nitaleta mvua ya mawe inyeshe kwa nguvu, nao upepo wa dhoruba utavuma juu yake. 12Wakati ukuta utakapoanguka, je, watu hawatawauliza, “Iko wapi chokaa mliyopaka ukuta?”
13 k“ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Katika ghadhabu yangu nitauachia upepo wa dhoruba, pia katika hasira yangu mvua ya mawe na mvua ya mafuriko itanyesha ikiwa na ghadhabu ya kuangamiza. 14 lNitaubomoa ukuta mlioupaka chokaa na kuuangusha chini ili msingi wake uachwe wazi. Utakapoanguka, mtaangamizwa ndani yake, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana. 15Hivyo ndivyo nitakavyoitimiza ghadhabu yangu dhidi ya huo ukuta na dhidi yao walioupaka chokaa. Nitawaambia ninyi, “Ukuta umebomoka na vivyo hivyo wale walioupaka chokaa, 16 mwale manabii wa Israeli waliotabiri juu ya Yerusalemu na kuona maono ya amani kwa ajili yake wakati kulipokuwa hakuna amani, asema Bwana Mwenyezi.” ’
17 n“Sasa, mwanadamu, kaza uso wako dhidi ya binti za watu wako wanaotabiri mambo kutoka mawazo yao wenyewe. Tabiri dhidi yao 18 ona useme, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ole wao wanawake washonao hirizi za uchawi juu ya viwiko vyao vyote na kutengeneza shela za urefu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufunika vichwa vyao kwa makusudi ya kuwanasa watu. Je, mtatega uhai wa watu wangu lakini ninyi mponye wa kwenu? 19 pNinyi mmeninajisi miongoni mwa watu wangu kwa ajili ya konzi chache za shayiri na chembe za mkate. Kwa kuwaambia uongo watu wangu, wale ambao husikiliza uongo, mmewaua wale watu ambao wasingekufa na kuwaacha hai wale ambao wasingeishi.
20 q“ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi niko kinyume na hizo hirizi zenu za uchawi ambazo kwa hizo mnawatega watu kama ndege, nami nitazirarua kutoka mikononi mwenu, nitawaweka huru watu wale mliowatega kama ndege. 21 rNitazirarua shela zenu na kuwaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu, nao hawatakuwa tena mawindo ya nguvu zenu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana. 22 sKwa sababu mliwavunja moyo wenye haki kwa uongo wenu, wakati mimi sikuwaletea huzuni na kwa kuwa mliwatia moyo waovu ili wasiziache njia zao mbaya na hivyo kuokoa maisha yao, 23 tkwa hiyo hamtaona tena maono ya uongo wala kufanya ubashiri. Nitawaokoa watu wangu kutoka mikononi mwenu. Nanyi ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”
Copyright information for
SwhNEN