Ezekiel 5:5-17
5 a“Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Huu ndio Yerusalemu ambao nimeuweka katikati ya mataifa ukiwa umezungukwa na nchi pande zote. 6 bLakini katika uovu wake umeasi sheria na amri zangu kuliko mataifa na nchi zinazouzunguka. Umeasi sheria zangu wala haukufuata amri zangu.7 c“Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ninyi mmekuwa wakaidi kuliko mataifa yanayowazunguka na hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu. Wala hamkuweza hata kuzifuata kawaida za mataifa yanayowazunguka.
8 d“Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo, Mimi mwenyewe, niko kinyume nanyi Yerusalemu, nitawapiga kwa adhabu yangu mbele ya mataifa. 9 eKwa ajili ya sanamu zenu zote za machukizo, nitawafanyia kile ambacho kamwe sijawafanyia kabla wala kamwe sitawafanyia tena. 10 fKwa hiyo katikati yenu baba watakula watoto wao na watoto watakula baba zao. Nitawapiga kwa adhabu, nami nitawatawanya watu wenu walionusurika pande zote za dunia. 11 gKwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, kwa kuwa mmenajisi mahali pangu patakatifu kwa sanamu zenu mbaya sana na desturi zenu za machukizo, mimi mwenyewe nitaondoa fadhili zangu kwenu. 12 hTheluthi ya watu wako watakufa kwa tauni au kwa njaa humu ndani yako, theluthi nyingine itaanguka kwa upanga nje ya kuta zako, nayo theluthi nyingine nitaitawanya kwenye pande nne kuwafuatia kwa upanga uliofutwa.
13 i“Ndipo hasira yangu itakapokoma na ghadhabu yangu dhidi yao itatulia, nami nitakuwa nimelipiza kisasi. Baada ya kuimaliza ghadhabu yangu juu yao, watajua kuwa mimi Bwana nimenena katika wivu wangu.
14 j“Nitakuangamiza na kukufanya kitu cha kudharauliwa miongoni mwa mataifa yanayokuzunguka, machoni pa watu wote wapitao karibu nawe. 15 kUtakuwa kitu cha kudharauliwa na cha aibu, cha dhihaka, ovyo na kitu cha kutisha kwa mataifa yanayokuzunguka, nitakapokupiga kwa adhabu yangu katika hasira na ghadhabu yangu kwa kukukemea kwa ukali. Mimi Bwana nimesema. 16 lNitakapokupiga kwa mishale yangu ya kufisha na yenye kuharibu ya njaa, nitaipiga ili kukuangamiza. Nitaleta njaa zaidi na zaidi juu yako na kukomesha upatikanaji wa chakula kwako. 17 mNitapeleka njaa na wanyama wa mwituni dhidi yenu, navyo vitawaacha bila watoto. Tauni na umwagaji wa damu utapita katikati yenu, nami nitaleta upanga juu yenu. Mimi Bwana nimenena haya.”
Copyright information for
SwhNEN