Hebrews 1
Mwana Ni Mkuu Kuliko Malaika
1 aZamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, 2 blakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu. 3 cMwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni. 4 dKwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.5 eKwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wowote Mungu alipata kumwambia,
“Wewe ni Mwanangu;
leo mimi nimekuzaa?”
Au tena,
“Mimi nitakuwa Baba yake,
naye atakuwa Mwanangu?”
6 fTena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema,
“Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”
7 gAnenapo kuhusu malaika asema,
“Huwafanya malaika wake kuwa pepo,
watumishi wake kuwa miali ya moto.”
8 hLakini kwa habari za Mwana asema,
“Kiti chako cha enzi, Ee Mungu,
kitadumu milele na milele,
nayo haki itakuwa fimbo ya utawala
ya ufalme wako.
9 iUmependa haki na kuchukia uovu;
kwa hiyo Mungu, Mungu wako,
amekuweka juu ya wenzako
kwa kukupaka mafuta ya furaha.”
10 jPia asema,
“Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia,
nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
11 kHizo zitatoweka, lakini wewe utadumu;
zote zitachakaa kama vazi.
12 lUtazikungʼutakungʼuta kama joho,
nazo zitachakaa kama vazi.
Lakini wewe hubadiliki,
nayo miaka yako haikomi kamwe.”
13 mJe, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wowote,
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako”?
14 nJe, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?
Copyright information for
SwhNEN