Hosea 14

Toba Iletayo Baraka

1 aRudi, ee Israeli, kwa Bwana Mungu wako.
Dhambi zako zimekuwa
ndilo anguko lako!
2 bChukueni maneno pamoja nanyi,
mkamrudie Bwana.
Mwambieni:
“Samehe dhambi zetu zote
na utupokee kwa neema,
ili tuweze kutoa matunda yetu
kama sadaka za mafahali.
3 cAshuru hawezi kutuokoa,
hatutapanda farasi wa vita.
Kamwe hatutasema tena ‘Miungu yetu’
kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza,
kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”

4 d“Nitaponya ukaidi wao
na kuwapenda kwa hiari yangu,
kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.
5 eNitakuwa kama umande kwa Israeli;
atachanua kama yungiyungi.
Kama mwerezi wa Lebanoni
atashusha mizizi yake chini;
6 fmatawi yake yatatanda.
Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni,
harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.
7 gWatu wataishi tena kwenye kivuli chake.
Atastawi kama nafaka.
Atachanua kama mzabibu,
nao umaarufu wake utakuwa
kama divai itokayo Lebanoni.
8 hEe Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu?
Nitamjibu na kumtunza.
Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi;
kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”

9 iNi nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya.
Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa.
Njia za Bwana ni adili;
wenye haki huenda katika njia hizo,
lakini waasi watajikwaa ndani yake.
Copyright information for SwhNEN