Isaiah 50

Dhambi Ya Israeli Na Utii Wa Mtumishi

1 aHili ndilo asemalo Bwana:

“Iko wapi hati ya talaka ya mama yako
ambayo kwayo niliachana naye?
Au nimewauza ninyi kwa nani
miongoni mwa watu wanaonidai?
Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa,
kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa.
2 bNilipokuja, kwa nini hakuwepo hata mmoja?
Nilipoita, kwa nini hakuwepo hata mmoja wa kujibu?
Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa?
Je, mimi sina nguvu za kukuokoa?
Kwa kukemea tu naikausha bahari,
naigeuza mito ya maji kuwa jangwa;
samaki wake wanaoza kwa kukosa maji
na kufa kwa ajili ya kiu.
3 cNinalivika anga weusi na kufanya nguo ya gunia
kuwa kifuniko chake.”

4 d Bwana Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa,
ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka.
Huniamsha asubuhi kwa asubuhi,
huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.
5 e Bwana Mwenyezi amezibua masikio yangu,
nami sikuwa mwasi,
wala sikurudi nyuma.
6 fNiliwapa mgongo wangu wale wanipigao,
mashavu yangu wale wangʼoao ndevu zangu;
sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha
na kutemewa mate.
7 gKwa sababu Bwana Mwenyezi ananisaidia,
sitatahayarika.
Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe la gumegume,
nami ninajua sitaaibika.
8 hYeye anipatiaye haki yangu yu karibu.
Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu?
Tukabiliane uso kwa uso!
Mshtaki wangu ni nani?
Ni nani aliye mshtaki wangu?
9 iNi Bwana Mwenyezi anisaidiaye mimi.
Ni nani huyo atakayenihukumu?
Wote watachakaa kama vazi,
nondo watawala wawamalize.

10 jNi nani miongoni mwenu amchaye Bwana,
na kulitii neno la mtumishi wake?
Yeye atembeaye gizani,
yeye asiye na nuru,
na alitumainie jina la Bwana,
na amtegemee Mungu wake.
11 kLakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto,
na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi,
nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu
na ya mienge mliyoiwasha.
Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu:
Mtalala chini kwa mateso makali.
Copyright information for SwhNEN