Jeremiah 30
Kurudishwa Kwa Israeli
1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana: 2 a“Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Andika katika kitabu maneno yote niliyonena na wewe. 3 bSiku zinakuja,’ asema Bwana, ‘nitakapowaleta watu wangu Israeli na Yuda kutoka uhamishoni, na kuwarudisha katika nchi niliyowapa baba zao ili kuimiliki,’ asema Bwana.”4Haya ndiyo maneno Bwana aliyoyanena kuhusu Israeli na Yuda: 5 c“Hili ndilo asemalo Bwana:
“ ‘Vilio vya woga vinasikika:
hofu kuu, wala si amani.
6 dUlizeni na mkaone:
Je, mwanaume aweza kuzaa watoto?
Kwa nini basi ninaona kila mwanaume mwenye nguvu
ameweka mikono yake tumboni
kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa,
kila uso ukigeuka rangi kabisa?
7 eTazama jinsi ile siku itakavyokuwa ya kutisha!
Hakutakuwa na nyingine mfano wake.
Utakuwa wakati wa dhiki kwa Yakobo,
lakini ataokolewa kutoka hiyo.
8 f“ ‘Katika siku ile,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote,
‘nitaivunja nira kutoka shingoni mwao
na kuvipasua vifungo vyao;
wageni hawatawafanya tena watumwa.
9 gBadala yake, watamtumikia Bwana, Mungu wao
na Daudi mfalme wao,
nitakayemwinua kwa ajili yao.
10 h“ ‘Hivyo usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,
usifadhaike, ee Israeli,’
asema Bwana.
‘Hakika, nitakuokoa kutoka mbali,
wazao wako kutoka nchi ya uhamisho wao.
Yakobo atakuwa tena na amani na usalama,
wala hakuna atakayemtia hofu.
11 iMimi niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,’
asema Bwana.
‘Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote
ambamo miongoni mwao nimewatawanya,
sitawaangamiza ninyi kabisa.
Nitawaadhibu, lakini kwa haki.
Sitawaacha kabisa bila adhabu.’
12 j“Hili ndilo asemalo Bwana:
“ ‘Kidonda chako hakina dawa,
jeraha lako haliponyeki.
13 kHakuna yeyote wa kukutetea shauri lako,
hakuna dawa ya kidonda chako,
wewe hutapona.
14 lWale walioungana nawe wote wamekusahau,
hawajali chochote kukuhusu wewe.
Nimekupiga kama vile adui angelifanya,
na kukuadhibu kama vile mtu mkatili angelifanya,
kwa sababu hatia yako ni kubwa mno
na dhambi zako ni nyingi sana.
15 mKwa nini unalia kwa ajili ya jeraha lako,
yale maumivu yako yasiyoponyeka?
Kwa sababu ya uovu wako mkubwa na dhambi zako nyingi
nimekufanyia mambo haya.
16 n“ ‘Lakini watu wote wakuangamizao wataangamizwa;
adui zako wote watakwenda uhamishoni.
Wale wote wakutekao nyara watatekwa nyara;
wote wakufanyao mateka nitawafanya mateka.
17 oLakini nitakurudishia afya yako
na kuyaponya majeraha yako,’
asema Bwana,
‘kwa sababu umeitwa mwenye kutupwa,
Sayuni ambaye hakuna yeyote anayekujali.’
18 p“Hili ndilo asemalo Bwana:
“ ‘Nitarudisha baraka za mahema ya Yakobo,
na kuhurumia maskani yake.
Mji utajengwa tena juu ya magofu yake,
nalo jumba la kifalme litasimama mahali pake halisi.
19 qNyimbo za kushukuru zitatoka kwao
na sauti ya furaha.
Nitaiongeza idadi yao
wala hawatapungua,
nitawapa heshima
na hawatadharauliwa.
20 rWatoto wao watakuwa kama walivyokuwa
siku za zamani,
nayo jumuiya yao itaimarishwa mbele yangu;
nitawaadhibu wale wote wawaoneao.
21 sMmoja wao atakuwa kiongozi wao;
mtawala wao atainuka miongoni mwao.
Nitamleta karibu nami,
naye atanikaribia mimi,
kwa maana ni nani yule atakayejitolea
kuwa karibu nami?’
asema Bwana.
22 t‘Kwa hiyo ninyi mtakuwa watu wangu,
nami nitakuwa Mungu wenu.’ ”
23 uTazama, tufani ya Bwana
italipuka kwa ghadhabu,
upepo wa kisulisuli uendao kasi
utashuka juu ya vichwa vya waovu.
24 vHasira kali ya Bwana haitarudi nyuma
mpaka atakapotimiza makusudi yote ya moyo wake.
Siku zijazo
mtayaelewa haya.
Copyright information for
SwhNEN