Job 20
Sofari Anasema: Uovu Hupokea Malipo Ya Haki
1 aNdipo Sofari Mnaamathi akajibu:2 b“Mawazo yanayonisumbua yananisukuma kujibu,
kwa sababu nimehangaika sana.
3 cNinasikia makaripio ambayo yananivunjia heshima,
nao ufahamu wangu unanisukuma kujibu.
4 d“Hakika unajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani,
tangu zamani mwanadamu alipowekwa duniani,
5 emacheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi,
nayo furaha ya wasiomcha Mungu hudumu kwa kitambo tu.
6 fIngawa kujikweza kwake hufikia mbinguni
na kichwa chake hugusa mawingu,
7 gataangamia milele kama mavi yake mwenyewe.
Wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’
8 hKama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena,
amefukuziwa mbali kama maono ya usiku.
9 iJicho lililomwona halitamwona tena;
mahali pake hapatamwona tena.
10 jWatoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini,
nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyangʼanya watu.
11 kNguvu za ujana zilizoijaza mifupa yake,
zitalala naye mavumbini.
12 l“Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake
naye huuficha chini ya ulimi wake,
13 mingawa hawezi kukubali kuuachia uende,
lakini huuweka kinywani mwake.
14 n oHata hivyo chakula chake kitakuwa kichungu tumboni mwake,
nacho kitakuwa sumu kali ya nyoka ndani yake.
15 pAtatema mali alizozimeza;
Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika.
16 qAtanyonya sumu za majoka;
meno ya nyoka mwenye sumu kali yatamuua.
17 rHatafurahia vijito,
mito inayotiririsha asali na siagi.
18 sVile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila;
hatafurahia faida itokanayo na biashara yake.
19 tKwa kuwa aliwaonea maskini na kuwaacha pasipo kitu;
amenyangʼanya kwa nguvu nyumba asizozijenga.
20 u“Hakika hatakuwa na raha katika kutamani kwake sana;
hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake.
21 vHakuna chochote kitakachosalia kwa ajili yake ili ale;
kufanikiwa kwake hakutadumu.
22 wKatikati ya wingi wa ustawi wake, dhiki itampata;
taabu itamjia kwa nguvu zote.
23 xAtakapokuwa amelijaza tumbo lake,
Mungu ataionyesha ghadhabu kali dhidi yake,
na kumnyeshea mapigo juu yake.
24 yIjapokuwa aikimbia silaha ya chuma,
mshale wa shaba utamchoma.
25 zAtauchomoa katika mgongo wake,
ncha ingʼaayo kutoka ini lake.
Vitisho vitakuja juu yake;
26 aagiza nene linavizia hazina zake.
Moto usiopepewa na mtu utamteketeza,
na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake.
27 abMbingu zitaweka wazi hatia yake,
nayo nchi itainuka kinyume chake.
28 acMafuriko yataichukua nyumba yake,
maji yaendayo kasi katika siku ya ghadhabu ya Mungu.
29 adHili ndilo fungu Mungu alilowagawia waovu,
urithi uliowekwa kwa ajili yao na Mungu.”
Copyright information for
SwhNEN