John 20:11-18
Yesu Anamtokea Maria Magdalene
(Mathayo 28:9-10; Marko 16:9-11)
11 aLakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini, 12 bnaye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.13 cWakamuuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?”
Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.” 14 dBaada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua.
15 eYesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”
Maria akidhani ya kuwa aliyekuwa anaongea naye ni mtunza bustani, kwa hiyo akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nionyeshe ulikomweka, nami nitamchukua.”
16 fYesu akamwita, “Maria!”
Ndipo Maria akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Rabboni!” (maana yake Mwalimu).
17 gYesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”
18 hKwa hiyo Maria Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Yesu alikuwa amemweleza mambo hayo yote.
Copyright information for
SwhNEN