Joshua 23
Yoshua Anawaaga Viongozi
1 aBaada ya muda mrefu kupita, naye Bwana akawa amewapa Israeli pumziko mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo akiwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana, 2 bakawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa Yoshua akawaambia: “Mimi ni mzee na umri wangu umeendelea sana. 3 cNinyi wenyewe mmeona kila kitu Bwana Mungu wenu, alichowatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Ilikuwa ni Bwana Mungu wenu aliyewapigania. 4 dKumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari kuu upande wa magharibi. 5 eBwana Mungu wenu mwenyewe atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile Bwana Mungu wenu alivyowaahidi.6 f“Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. 7 gMsishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. 8 hBali mtashikamana kwa uthabiti na Bwana, Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa.
9 i“Bwana amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, mpaka siku ya leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu. 10 jMtu mmoja miongoni mwenu anafukuza watu elfu, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anawapigania, kama alivyoahidi. 11 kKwa hiyo kuweni waangalifu sana kumpenda Bwana Mungu wenu.
12 l“Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia katikati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, 13 mbasi mwe na hakika kuwa Bwana Mungu wenu hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu, na miiba machoni mwenu, mpaka mwangamie kutoka nchi hii nzuri, ambayo Bwana Mungu wenu amewapa.
14 n“Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema Bwana Mungu wenu alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. 15 oLakini kama vile kila ahadi njema ya Bwana Mungu wenu imekuwa kweli, vivyo hivyo Bwana ataleta maovu yote kama alivyo onya, mpaka awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa. 16 pKama mkilivunja agano la Bwana Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya Bwana itawaka dhidi yenu, nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”
Copyright information for
SwhNEN