Psalms 107

KITABU CHA TANO

(Zaburi 107–150)

Kumsifu Mungu Kwa Wema Wake

1 aMshukuruni Bwana, kwa kuwa yeye ni mwema,
upendo wake wadumu milele.
2 bWaliokombolewa wa Bwana na waseme hivi,
wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,
3 cwale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali,
kutoka mashariki na magharibi,
kutoka kaskazini na kusini.

4 dBaadhi yao walitangatanga jangwani,
hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi.
5 eWalikuwa na njaa na kiu,
nafsi zao zikadhoofika.
6 fNdipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
7 gAkawaongoza kwa njia iliyo sawa
hadi mji ambao wangeweza kuishi.
8 hBasi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
9 ikwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu,
na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.

10 jWengine walikaa gizani na katika huzuni kuu,
wafungwa wakiteseka katika minyororo,
11 kkwa sababu walikuwa wameasi
dhidi ya maneno ya Mungu
na kudharau shauri
la Aliye Juu Sana.
12 lAliwatumikisha kwa kazi ngumu;
walijikwaa na hapakuwepo yeyote wa kuwasaidia.
13 mNdipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
14 nAkawatoa katika giza na huzuni kuu
na akavunja minyororo yao.
15 oBasi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
16 pkwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba
na kukata mapingo ya chuma.

17 qWengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao,
wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao.
18 rWakachukia kabisa vyakula vyote,
wakakaribia malango ya mauti.
19 sNdipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawaokoa kutoka taabu yao.
20 tAkalituma neno lake na kuwaponya,
akawaokoa kutoka maangamizo yao.
21 uBasi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
22 vNa watoe dhabihu za kushukuru,
na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.

23 wWengine walisafiri baharini kwa meli,
walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu.
24 xWaliziona kazi za Bwana,
matendo yake ya ajabu kilindini.
25 yKwa maana alisema na kuamsha tufani
iliyoinua mawimbi juu.
26 zYakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini,
katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka.
27 aaWalipepesuka na kuyumbayumba kama walevi,
ujanja wao ukafikia ukomo.
28 abNdipo walipomlilia Bwana katika shida yao,
naye akawatoa kwenye taabu yao.
29 acAkatuliza dhoruba kwa mnongʼono,
mawimbi ya bahari yakatulia.
30 adWalifurahi ilipokuwa shwari,
naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani.
31 aeBasi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,
na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
32 afNa wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu,
na wamsifu katika baraza la wazee.

33 agYeye aligeuza mito kuwa jangwa,
chemchemi za maji zitiririkazo kuwa ardhi yenye kiu,
34 ahnchi izaayo ikawa ya chumvi isiyofaa,
kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo.
35 aiAligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji,
nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zitiririkazo;
36 ajaliwaleta wenye njaa wakaishi humo,
nao wakajenga mji wangeweza kuishi.
37 akWalilima mashamba na kupanda mizabibu,
nayo ikazaa matunda mengi,
38 alMungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana,
wala hakuruhusu mifugo yao kupungua.

39 amKisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa
kwa kuonewa, maafa na huzuni.
40 anYeye ambaye huwamwagia dharau wakuu,
aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia.
41 aoLakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao,
na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo.
42 apWanyofu wataona na kufurahi,
lakini waovu wote watafunga vinywa vyao.

43 aqYeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya,
na atafakari upendo mkuu wa Bwana.
Copyright information for SwhNEN