Psalms 90

KITABU CHA NNE

(Zaburi 90–106)

Umilele Wa Mungu Na Udhaifu Wa Mwanadamu

Maombi ya Mose, mtu wa Mungu.

1 a Bwana, wewe umekuwa makao yetu
katika vizazi vyote.
2 bKabla ya kuzaliwa milima
au hujaumba dunia na ulimwengu,
wewe ni Mungu tangu milele hata milele.

3 cHuwarudisha watu mavumbini,
ukisema, “Rudini mavumbini, enyi wanadamu.”
4 dKwa maana kwako miaka elfu
ni kama siku moja iliyokwisha pita,
au kama kesha la usiku.
5 eUnawatowesha wanadamu katika usingizi wa kifo,
nao ni kama majani machanga ya asubuhi:
6 fingawa asubuhi yanachipua,
ifikapo jioni huwa yamenyauka na kukauka.

7Tumeangamizwa kwa hasira yako
na tumetishwa kwa ghadhabu yako.
8 gUmeyaweka maovu yetu mbele yako,
dhambi zetu za siri katika nuru ya uwepo wako.
9 hTumeishi siku zetu zote chini ya ghadhabu yako,
tunamaliza miaka yetu kwa kuomboleza.
10 iSiku zetu za kuishi ni miaka sabini,
au miaka themanini ikiwa tuna nguvu,
lakini yote ni ya shida na taabu,
nazo zapita haraka, nasi twatoweka.

11 jNi nani ajuaye nguvu za hasira yako?
Kwa maana ghadhabu yako ni kubwa
kama hofu tunayopaswa kuwa nayo kwako.
12 kTufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri,
ili tujipatie moyo wa hekima.

13 lEe Bwana, uwe na huruma! Utakawia hata lini?
Wahurumie watumishi wako.
14 mTushibishe asubuhi kwa upendo wako usiokoma,
ili tuweze kuimba kwa shangwe na kufurahi siku zetu zote.
15Utufurahishe kulingana na siku ulizotuadhibu,
kulingana na miaka tuliyotaabika.
16 nMatendo yako na yaonekane kwa watumishi wako,
utukufu wako kwa watoto wao.

17 oWema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu;
uzithibitishe kazi za mikono yetu:
naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu.
Copyright information for SwhNEN