Song of Solomon 4

Mpenzi

1 aTazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Ee, jinsi ulivyo mzuri!
Macho yako nyuma ya shela yako
ni kama ya hua.
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi
zikishuka kutoka Mlima Gileadi.
2 bMeno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi,
watokao kuogeshwa.
Kila mmoja ana pacha lake,
hakuna hata mmoja aliye peke yake.
3 cMidomo yako ni kama uzi mwekundu,
kinywa chako kinapendeza.
Mashavu yako nyuma ya shela yako
ni kama vipande viwili vya komamanga.
4 dShingo yako ni kama mnara wa Daudi,
uliojengwa kwa madaha,
juu yake zimetundikwa ngao elfu,
zote ni ngao za mashujaa.
5 eMatiti yako mawili ni kama wana-paa wawili,
kama wana-paa mapacha
wajilishao katikati ya yungiyungi.
6 fHata kupambazuke na vivuli vikimbie,
nitakwenda kwenye mlima wa manemane
na kwenye kilima cha uvumba.
7 gWewe ni mzuri kote, mpenzi wangu,
hakuna hitilafu ndani yako.

8 hEnda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu,
enda nami kutoka Lebanoni.
Shuka kutoka ncha ya Amana,
kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni,
kutoka mapango ya simba
na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.
9 iUmeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu;
umeiba moyo wangu
kwa mtazamo mmoja wa macho yako,
kwa kito kimoja cha mkufu wako.
10 jTazama jinsi pendo lako linavyofurahisha,
dada yangu, bibi arusi wangu!
Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai,
na harufu ya manukato yako zaidi ya kikolezo chochote!
11 kMidomo yako inadondosha utamu kama sega la asali,
bibi arusi wangu;
maziwa na asali viko chini ya ulimi wako.
Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.
12 lWewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu,
bibi arusi wangu;
wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa,
chemchemi yangu peke yangu.
13 mMimea yako ni bustani ya mikomamanga
yenye matunda mazuri sana,
yenye hina na nardo,
14 nnardo na zafarani,
mchai na mdalasini,
pamoja na kila aina ya mti wa uvumba,
manemane na udi,
na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote.
15 oWewe ni chemchemi ya bustani,
kisima cha maji yatiririkayo,
yakitiririka kutoka Lebanoni.
Mpendwa

16 pAmka, upepo wa kaskazini,
na uje, upepo wa kusini!
Vuma juu ya bustani yangu,
ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ngʼambo.
Mpendwa wangu na aje bustanini mwake
na kuonja matunda mazuri sana.
Copyright information for SwhNEN