Joshua 17:1-6

Mgawo Wa Nusu Nyingine Ya Manase Upande Wa Magharibi

1 aHuu ndio mgawo wa kabila la Manase kama mzaliwa wa kwanza wa Yusufu, yaani kwa ajili ya Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase. Makiri alikuwa baba wa Wagileadi, ambao walipokea Gileadi na Bashani kwa sababu Wamakiri walikuwa askari wakuu. 2 bKwa hiyo mgawo huu ulikuwa kwa ajili ya watu wa Manase waliokuwa wamebaki, ambao ni koo za Abiezeri, Heleki, Asirieli, Shekemu, Heferi na Shemida. Hawa ndio wanaume wale wengine wa uzao wa Manase mwana wa Yusufu kwa koo zao.

3 cBasi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana waume ila mabinti tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. 4 dWakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “Bwana alimwagiza Musa atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo la Bwana. 5 eFungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi, licha ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani, 6kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi miongoni mwa wana wa kiume. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wazao wa Manase waliobaki.
Copyright information for SwhKC