‏ 2 Chronicles 17

Yehoshafati Mfalme Wa Yuda

1Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake na akajiimarisha dhidi ya Israeli. 2Akaweka jeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome na kuweka askari walinzi katika Yuda na katika miji ya Efraimu ile ambayo baba yake Asa alikuwa ameiteka.

3 Bwana Mungu alikuwa na Yehoshafati kwa sababu katika miaka yake ya mwanzoni alienenda katika njia za Daudi baba yake. Hakutafuta Mabaali 4bali alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzifuata amri zake badala ya kufuata desturi za watu wa Israeli. 5Kwa hiyo Bwana akauimarisha ufalme chini ya uongozi wake, nao Yuda wote wakamletea Yehoshafati zawadi, hivyo akawa na utajiri mwingi na heshima. 6Moyo wake ukawa hodari katika njia za Bwana na zaidi ya yote, akaondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu na nguzo za Maashera katika Yuda.

7Katika mwaka wa tatu wa utawala wa akatuma maafisa wake ambao ni: Ben-Haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya ili kufundisha katika miji ya Yuda. 8Pamoja nao walikuwepo Walawi fulani nao ni: Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia, Tob-Adonia, pamoja nao walikuwepo makuhani Elishama na Yehoramu. 9Wakafundisha Yuda yote, wakiwa wamechukua Kitabu cha Sheria ya Bwana wakazunguka miji yote ya Yuda na kufundisha watu.

10Hofu ya Bwana ikawa juu ya falme zote za nchi zilizozunguka Yuda, hivyo hawakufanya vita na Yehoshafati. 11Baadhi ya Wafilisti wakamletea Yehoshafati zawadi na fedha kama ushuru, nao Waarabu wakamletea mifugo: kondoo dume 7,700 na mbuzi 7,700.

12Yehoshafati akaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi, akajenga ngome na miji ya hazina katika Yuda 13na akawa na wingi mkubwa wa vitu katika miji ya Yuda. Pia aliweka askari wa vita wenye uzoefu huko Yerusalemu. 14Wakaandikishwa katika jamaa zao kama ifuatavyo:

Kutoka Yuda, majemadari wa vikosi vya elfu:
Jemadari Adna akiwa na askari wa vita 300,000;
15aliyefuata ni jemadari Yehohanani, akiwa na askari 280,000 walio tayari kwa vita;
16aliyefuata ni Amasia mwana wa Zikri, ambaye alijitolea kwa ajili ya kazi ya Bwana, akiwa na askari 200,000.
17Kutoka Benyamini:
Eliada, askari shujaa akiwa na watu 200,000 wenye silaha za nyuta na ngao;
18aliyefuata ni Yehozabadi, akiwa na askari 180,000 wenye silaha za vita.

19Hawa ndio waliomtumikia mfalme, mbali na wale mfalme aliweka katika miji yenye ngome huko Yuda yote.
Copyright information for SwhNeno