‏ 2 Samuel 22

Wimbo Wa Daudi Wa Sifa

(Zaburi 18)

1Daudi alimwimbia Bwana maneno ya wimbo huu wakati Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. 2Akasema: Bwana ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
3Mungu wangu ni mwamba wangu,
ambaye kwake ninakimbilia,
ngao yangu na pembe ya wokovu wangu.
Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu
na mwokozi wangu,
huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.
4Ninamwita Bwana, anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.

5“Mawimbi ya mauti yalinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
6Kamba za kuzimu
Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, maana yake ni Shimo lisilo na mwisho.
zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
7Katika shida yangu nalimwita Bwana,
nilimlilia Mungu wangu.
Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika masikioni mwake.

8“Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya mbingu ikatikisika,
vilitetemeka kwa sababu
alikuwa amekasirika.
9Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yawakayo
yakatoka ndani mwake.
10Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
11Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mbawa za upepo.
12Alifanya giza hema lake la kujifunika:
mawingu meusi ya mvua ya angani.
13Kutokana na mwanga wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikanyesha mvua ya mawe
na umeme wa radi.
14 Bwana alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
15Aliipiga mishale na kutawanya adui,
umeme wa radi na kuwafukuza.
16Mabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwake Bwana,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.

17“Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
18Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
19Walinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Bwana alikuwa msaada wangu.
20Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.

21Bwana alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
22Kwa maana nimezishika njia za Bwana;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
23Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
24Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
25 Bwana amenilipa sawasawa na uadilifu wangu,
sawasawa na usafi wangu machoni pake.

26“Kwa yeye aliye mwaminifu unajionyesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia unajionyesha kutokuwa na hatia,
27kwa aliye mtakatifu unajionyesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka unajionyesha kuwa mkaidi.
28Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi
ili uwashushe.
29Wewe ni taa yangu, Ee Bwana.
Bwana hulifanya giza langu
kuwa mwanga.
30Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.

31“Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu;
neno la Bwana halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
32Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Bwana?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
33Mungu ndiye anivikaye nguvu
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
34Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
35Huifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
36Hunipa ngao yako ya ushindi,
unajishusha chini ili kuniinua.
37Huyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.

38“Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta,
sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.
39Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
41Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
42Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa;
walimlilia Bwana, lakini hakuwajibu.
43Niliwaponda kama mavumbi ya nchi;
niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani.

44“Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu;
umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa.
Watu ambao sikuwajua wananitumikia,
45nao wageni huja wakininyenyekea,
mara wanisikiapo, hunitii.
46Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.

47Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu,
Mwamba, Mwokozi wangu!
48Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
ayawekaye mataifa chini yangu,
49aniwekaye huru toka kwa adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
50Kwa hiyo nitakusifu, Ee Bwana,
katikati ya mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.
51Humpa mfalme wake ushindi mkuu;
huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.”
Copyright information for SwhNeno