Exodus 15
Wimbo Wa Mose Na Miriamu
1Ndipo Mose na Waisraeli wakamwimbia Bwana wimbo huu: “Nitamwimbia Bwana,kwa kuwa ametukuzwa sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.
2 Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,
Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
3 Bwana ni shujaa wa vita;
Bwana ndilo jina lake.
4Magari ya vita ya Farao na jeshi lake
amewatosa baharini.
Maafisa wa Farao walio bora sana
wamezamishwa katika Bahari ya Shamu.
5Maji yenye kina yamewafunika,
wamezama mpaka vilindini kama jiwe.
6“Mkono wako wa kuume, Ee Bwana
ulitukuka kwa uweza.
Mkono wako wa kuume, Ee Bwana,
ukamponda adui.
7Katika ukuu wa utukufu wako,
ukawaangusha chini wale waliokupinga.
Uliachia hasira yako kali,
ikawateketeza kama kapi.
8Kwa pumzi ya pua zako
maji yalijilundika.
Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta,
vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.
9“Adui alijivuna,
‘Nitawafuatia, nitawapata.
Nitagawanya nyara;
nitajishibisha kwa wao.
Nitafuta upanga wangu
na mkono wangu utawaangamiza.’
10Lakini ulipuliza kwa pumzi yako,
bahari ikawafunika.
Wakazama kama risasi
kwenye maji makuu.
11“Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Bwana?
Ni nani kama Wewe:
uliyetukuka katika utakatifu,
utishaye katika utukufu,
ukitenda maajabu?
12Uliunyoosha mkono wako wa kuume
na nchi ikawameza.
13“Katika upendo wako usiokoma utawaongoza
watu uliowakomboa.
Katika nguvu zako utawaongoza
mpaka makao yako matakatifu.
14Mataifa watasikia na kutetemeka,
uchungu utawakamata watu wa Ufilisti.
15Wakuu wa Edomu wataogopa,
viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu,
watu wa Kanaani watayeyuka,
16vitisho na hofu vitawaangukia.
Kwa nguvu ya mkono wako
watatulia kama jiwe,
mpaka watu wako waishe kupita, Ee Bwana,
mpaka watu uliowanunua wapite.
17Utawaingiza na kuwapandikiza
juu ya mlima wa urithi wako:
hapo mahali, Ee Bwana, ulipopafanya kuwa makao yako,
mahali patakatifu, Ee Bwana, ulipopajenga kwa mikono yako.
18 Bwana atatawala
milele na milele.”
19Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini, Bwana aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini wana wa Israeli walipita baharini mahali pakavu. 20Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Aroni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza. 21Miriamu akawaimbia: “Mwimbieni Bwana,
kwa maana ametukuka sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.”
Maji Ya Mara Na Elimu
22Kisha Mose akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji. 23Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara ▼▼Mara maana yake ni Chungu.
) 24Kwa hiyo watu wakamnungʼunikia Mose, wakisema, “Tunywe nini?” 25Ndipo Mose akamlilia Bwana, naye Bwana akamwonyesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu. Huko Bwana akawapa amri na sheria na huko akawajaribu. 26Mungu akasema, “Kama mkisikiliza kwa bidii sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yaliyo sawa machoni pake, kama mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, niwaponyaye.” 27Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.
Copyright information for
SwhNeno