‏ Job 28

Mapumziko: Imani Inakopatikana

1“Kuna machimbo ya fedha,
na mahali dhahabu isafishwapo.
2Chuma hupatikana ardhini,
nayo shaba huyeyushwa kutoka mawe ya madini.
3Mwanadamu hukomesha giza;
huyatafuta hadi sehemu iliyo mbali,
kwa ajili ya kuchimbua mawe yenye madini
katika giza jeusi sana.
4Huchimba shimo jembamba mbali na makao ya watu,
mahali paliposahaulika na nyayo za wanadamu;
mbali na wanadamu huningʼinia na kupembea kwa kamba.
5Ardhi, ambako chakula hutoka,
chini hugeuzwa kwa moto;
6yakuti samawi hutoka katika miamba yake,
nalo vumbi lake lina vipande vya dhahabu.
7Hakuna ndege awindaye aijuaye njia ile iliyofichika,
wala hakuna jicho la mwewe lililoiona.
8Wanyama wa porini wanaotamba hawajawahi kupakanyaga,
wala simba azungukaye huko.
9Mikono ya mwanadamu hushambulia miamba migumu sana,
na kuiacha wazi mizizi ya milima.
10Hutoboa shimo refu la kupenya chini kwa chini kwenye miamba;
macho yake huona hazina zake zote.
11Hutafuta vyanzo vya mito
na kuvileta vitu vilivyofichika katika nuru.

12“Lakini hekima inaweza kupatikana wapi?
Ufahamu unakaa wapi?
13Mwanadamu hatambui thamani yake;
haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai.
14Kilindi husema, ‘Haiko ndani yangu’;
bahari nayo husema, ‘Haiko pamoja nami.’
15Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote,
wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha.
16Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri,
kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa.
17Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo,
wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu.
18Marijani na yaspi hazistahili kutajwa;
thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu.
19Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo,
wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi.

20“Ni wapi basi hekima itokako?
Ufahamu hukaa wapi?
21Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai,
imesitiriwa hata kwa ndege wa angani.
22Uharibifu na Mauti husema,
‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’
23Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima
na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa,
24kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia
na huona kila kitu chini ya mbingu.
25Alipofanyiza nguvu za upepo
na kuyapima maji,
26alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua
na njia kwa ajili ya umeme wa radi,
27ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake,
akaithibitisha na kuihakikisha.
28Naye Mungu akamwambia mwanadamu,
‘Kumcha Bwana: hiyo ndiyo hekima,
nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’ ”
Copyright information for SwhNeno