‏ Job 29

Ayubu Anamaliza Utetezi Wake

1Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema: 2“Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita,
zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,
3wakati taa yake iliniangazia kichwani changu,
na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza!
4Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu,
wakati urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu,
5wakati Mwenyezi alikuwa pamoja nami,
nao watoto wangu walikuwa wamenizunguka,
6wakati njia yangu ilikuwa imenyweshewa siagi,
nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.

7“Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji
na kuketi katika kiwanja,
8vijana waliniona wakakaa kando,
nao wazee walioketi wakasimama;
9wakuu wakaacha kuzungumza
na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao;
10wenye vyeo wakanyamazishwa,
nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.
11Yeyote aliyenisikia alinena mema juu yangu,
nao walioniona walinisifu,
12kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada,
naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.
13Mtu aliyekuwa karibu kufa alinibariki,
nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.
14Niliivaa haki kama vazi langu;
uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.
15Nilikuwa macho ya kipofu
na miguu kwa kiwete.
16Nilikuwa baba kwa mhitaji;
nilimtetea mgeni.
17Niliyavunja meno makali ya waovu,
na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.

18“Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe,
nazo siku zangu zitakuwa nyingi kama chembechembe za mchanga.
19Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji,
nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.
20Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu,
upinde wangu daima utaendelea kuwa mpya mkononi mwangu.’

21“Watu walinisikiliza kwa tumaini,
wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.
22Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi;
maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.
23Waliningojea kama manyunyu ya mvua
na kuyapokea maneno yangu
kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.
24Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha;
nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.
25Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao;
niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake;
nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.
Copyright information for SwhNeno