‏ Job 36

Elihu Atukuza Wema Wa Mungu

1Elihu akaendelea kusema: 2“Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonyesha
kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.
3Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali,
nami nitamhesabia haki Muumba wangu.
4Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo;
mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.

5“Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu;
ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika shauri lake.
6Hawaachi waovu waendelee kuishi,
bali huwapa walioteswa haki yao.
7Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki;
huwaketisha penye viti vya enzi pamoja na wafalme
na kuwatukuza milele.
8Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo,
wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,
9huwaonyesha yale waliyoyatenda,
kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.
10Huwafanya wao kusikia maonyo,
na huwaagiza kutubu uovu wao.
11Kama wakitii na kumtumikia,
wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio,
na miaka yao katika utoshelevu.
12Lakini wasiposikiliza,
wataangamia kwa upanga,
nao watakufa pasipo maarifa.

13“Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki;
hata anapowafunga, hawamwombi msaada.
14Wanakufa wangali vijana,
miongoni mwa wanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu.
15Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao,
na kuzungumza nao katika dhiki zao.

16“Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki,
ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi,
hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.
17Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu;
hukumu na haki vimekukamata.
18Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri;
usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.
19Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi
vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?
20Usiutamani usiku uje,
ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.
21Jihadhari usigeukie uovu,
ambao unaupenda zaidi kuliko mateso.

22“Mungu ametukuzwa katika nguvu zake.
Ni nani aliye mwalimu kama yeye?
23Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake,
au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?
24Kumbuka kuzitukuza kazi zake,
ambazo watu wamezisifu katika wimbo.
25Wanadamu wote wameiona;
watu wanaikazia macho kwa mbali.
26Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu,
kupita ufahamu wetu!
Hesabu ya miaka yake haitafutiki.

27“Yeye huvuta juu matone ya maji,
ayachujayo kama mvua kutoka kwenye vijito;
28mawingu huangusha chini maji yake,
nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.
29Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu,
jinsi angurumavyo kutoka hemani mwake.
30Tazama jinsi anavyotandaza umeme wa radi kumzunguka,
naye huvifunika vilindi vya bahari.
31Hivi ndivyo atawalavyo mataifa,
na kuwapa chakula kwa wingi.
32Huujaza mkono wake kwa umeme wa radi,
na kuuagiza kulenga shabaha yake.
33Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja;
hata mifugo hujulisha kukaribia kwake.
Au: hutangaza kuja kwake.

Copyright information for SwhNeno