Job 38
Sehemu Ya Nne: Mungu Anazungumza
(Ayubu 38–41)
Bwana Anamjibu Ayubu
1Kisha Bwana akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema: 2“Nani huyu atiaye mashauri yangu gizakwa maneno yasiyo na maarifa?
3Jikaze kama mwanaume;
nitakuuliza swali,
nawe unijibu.
4“Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia?
Niambie, kama unafahamu.
5Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake?
Hakika wewe unajua!
Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?
6Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini,
au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,
7wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja,
na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?
8“Ni nani aliyeifungia bahari milango
ilipopasuka kutoka tumbo,
9nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake,
na kuyafungia katika giza nene,
10nilipoamuru mipaka yake,
na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,
11niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi;
hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?
12“Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke,
au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,
13yapate kushika miisho ya dunia,
na kuwakungʼuta waovu waliomo?
14Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri;
sura yake hukaa kama ile ya vazi.
15Waovu huzuiliwa nuru yao,
nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.
16“Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari?
Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?
17Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti?
Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?
18Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia?
Niambie kama unajua haya yote.
19“Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi?
Nako maskani mwa giza ni wapi?
20Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake?
Unajua njia za kufika maskani mwake?
21Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa!
Kwani umeishi miaka mingi!
22“Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji,
au kuona ghala za mvua ya mawe,
23ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu,
na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?
24Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa,
au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?
25Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi
na njia ya umeme wa radi,
26ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,
jangwa lisilo na yeyote ndani yake,
27ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa,
na majani yaanze kumea ndani yake?
28Je, mvua ina baba?
Ni nani baba azaaye matone ya umande?
29Barafu inatoka tumbo la nani?
Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,
30wakati maji yawapo magumu kama jiwe,
wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?
31“Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia?
Waweza kulegeza kamba za Orioni?
32Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake,
au kuongoza Dubu na watoto wake?
33Je, unajua sheria zinazotawala mbingu?
Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?
34“Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni,
na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?
35Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake?
Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?
36Ni nani aliyeujalia moyo hekima
au kuzipa akili ufahamu?
37Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu?
Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni
38wakati mavumbi yawapo magumu,
na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?
39“Je, utamwindia simba jike mawindo,
na kuwashibisha simba wenye njaa
40wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao,
au wakivizia kichakani?
41Ni nani ampaye kunguru chakula
wakati makinda yake yanamlilia Mungu,
yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?
Copyright information for
SwhNeno