Proverbs 2
Faida Za Hekima
1Mwanangu, kama utayakubali maneno yanguna kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
2kutega sikio lako kwenye hekima
na kuweka moyo wako katika ufahamu,
3na kama ukiita busara
na kuita kwa sauti ufahamu,
4na kama utaitafuta kama fedha
na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
5ndipo utakapoelewa kumcha Bwana
na kupata maarifa ya Mungu.
6Kwa maana Bwana hutoa hekima,
na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
7Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,
yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
8kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki
na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
9Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki
na sawa: yaani kila njia nzuri.
10Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako,
nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.
11Busara itakuhifadhi
na ufahamu utakulinda.
12Hekima itakuokoa kutoka njia za waovu,
kutoka kwa watu ambao maneno yao yamepotoka,
13wale waachao mapito yaliyonyooka
wakatembea katika njia za giza,
14wale wapendao kutenda mabaya
na kufurahia upotovu wa ubaya,
15ambao mapito yao yamepotoka
na ambao ni wapotovu katika njia zao.
16Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba,
kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno
ya kushawishi kutenda ubaya,
17aliyemwacha mwenzi wa ujana wake
na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu.
18Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo
na mapito yake kwenye roho za waliokufa.
19Hakuna yeyote aendaye kwake akarudi,
au kufikia mapito ya uzima.
20Hivyo utatembea katika njia za watu wema
na kushikamana na mapito ya wenye haki.
21Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi,
nao wasio na lawama watabakia ndani yake.
22Bali waovu watakatiliwa mbali kutoka nchi,
nao wasio waaminifu watangʼolewa kutoka humo.
Copyright information for
SwhNeno