Psalms 142
Maombi Ya Kuokolewa Dhidi Ya Watesi
Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Maombi. 1Namlilia Bwana kwa sauti,nainua sauti yangu kwa Bwana anihurumie.
2Namimina malalamiko yangu mbele zake,
mbele zake naeleza shida zangu.
3Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu,
wewe ndiwe unajua njia zangu.
Katika njia ninayopita
watu wameniwekea mtego.
4Tazama kuume kwangu na uone,
hakuna hata mmoja anayejihusisha nami.
Sina kimbilio,
hakuna anayejali maisha yangu.
5Ee Bwana, nakulilia wewe,
nasema, “Wewe ni kimbilio langu,
fungu langu katika nchi ya walio hai.”
6Sikiliza kilio changu,
kwa sababu mimi ni mhitaji sana;
niokoe na wale wanaonifuatilia,
kwa kuwa wamenizidi nguvu.
7Nifungue kutoka kifungo changu,
ili niweze kulisifu jina lako.
Ndipo wenye haki watanizunguka,
kwa sababu ya wema wako kwangu.
Copyright information for
SwhNeno