‏ Psalms 88

Kilio Kwa Ajili Ya Kuomba Msaada

Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi leanothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi.

1Ee Bwana, Mungu uniokoaye,
nimelia mbele zako usiku na mchana.
2Maombi yangu yafike mbele zako,
utegee kilio changu sikio lako.

3Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,
na maisha yangu yanakaribia kaburi.
Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.

4Nimehesabiwa miongoni mwa wale waendao shimoni,
niko kama mtu asiye na nguvu.
5Nimetengwa pamoja na wafu,
kama waliochinjwa walalao kaburini,
ambao huwakumbuki tena,
ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.

6Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana,
katika vina vya giza nene.
7Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu,
umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.

8Umenitenga na rafiki zangu wa karibu
na kunifanya chukizo kwao.
Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka;
9nuru ya macho yangu
imefifia kwa ajili ya huzuni.

Ee Bwana, ninakuita kila siku,
ninakunyooshea wewe mikono yangu.
10Je, wewe huwaonyesha wafu maajabu yako?
Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?

11Je, upendo wako hutangazwa kaburini,
uaminifu wako katika Uharibifu?
Yaani Abadon.

12Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza,
au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?

13Lakini ninakulilia wewe, Ee Bwana, unisaidie;
asubuhi maombi yangu huja mbele zako.
14Ee Bwana, kwa nini unanikataa
na kunificha uso wako?

15Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo;
nimepatwa na hofu zako, nami nimekata tamaa.
16Ghadhabu yako imepita juu yangu;
hofu zako zimeniangamiza.
17Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko;
zimenimeza kabisa.
18Umeniondolea marafiki na wapendwa wangu;
giza limekuwa ndilo rafiki yangu wa karibu kuliko wote.
Copyright information for SwhNeno