‏ Psalms 21

Shukrani Kwa Mungu Kwa Ajili Ya Ushindi

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1Ee Bwana, mfalme huzifurahia nguvu zako.
Tazama jinsi ilivyo kuu furaha yake
kwa ushindi unaompa!
2Umempa haja ya moyo wake
na hukumzuilia maombi ya midomo yake.
3Ulimkaribisha kwa baraka tele
na kumvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
4Alikuomba maisha, nawe ukampa,
wingi wa siku milele na milele.
5Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa,
umeweka juu yake fahari na utukufu.
6Hakika umempa baraka za milele,
umemfanya awe na furaha
kwa shangwe ya uwepo wako.
7Kwa kuwa mfalme anamtumaini Bwana;
kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.

8Mkono wako utawashika adui zako wote,
mkono wako wa kuume utawakamata adui zako.
9Wakati utakapojitokeza
utawafanya kama tanuru ya moto.
Katika ghadhabu yake Bwana atawameza,
moto wake utawateketeza.
10Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani,
uzao wao kutoka wanadamu.
11Ingawa watapanga mabaya dhidi yako
na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa,
12kwa kuwa utawafanya wakimbie
utakapowalenga usoni pao
kwa mshale kutoka kwenye upinde wako.

13Ee Bwana, utukuzwe katika nguvu zako,
tutaimba na kusifu nguvu zako.
Copyright information for SwhNeno