Psalms 22
Kilio Cha Uchungu Na Wimbo Wa Sifa
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri.” Zaburi ya Daudi. 1Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa?
Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?
2Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu,
hata usiku, sinyamazi.
3Hata hivyo umesimikwa katika kiti cha enzi kama Uliye Mtakatifu;
wewe ni sifa ya Israeli. ▼
▼Tafsiri zingine zinasema: uketiye juu ya sifa za Israeli.
4Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao,
walikutumaini nawe ukawaokoa.
5Walikulilia wewe na ukawaokoa,
walikutegemea wewe nao hawakuaibika.
6Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu,
wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau.
7Wote wanionao hunidhihaki,
hunivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao:
8Husema, “Anamtegemea Bwana,
basi Bwana na amwokoe.
Amkomboe basi, kwa maana
anapendezwa naye.”
9Hata hivyo ulinitoa tumboni,
ukanifanya nikutegemee,
hata nilipokuwa ninanyonya
matiti ya mama yangu.
10Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa,
toka tumboni mwa mama yangu
umekuwa Mungu wangu.
11Usiwe mbali nami,
kwa maana shida iko karibu
na hakuna wa kunisaidia.
12Mafahali wengi wamenizunguka,
mafahali wa Bashani wenye nguvu
wamenizingira.
13Simba wangurumao wanaorarua mawindo
yao hupanua vinywa vyao dhidi yangu.
14Nimemiminwa kama maji,
mifupa yangu yote imetoka katika viungo vyake.
Moyo wangu umegeuka kuwa nta,
umeyeyuka ndani yangu.
15Nguvu zangu zimekauka kama kigae,
ulimi wangu umegandamana
na kaakaa la kinywa changu,
kwa sababu umenilaza
katika mavumbi ya kifo.
16Mbwa wamenizunguka,
kundi la watu waovu limenizingira,
wametoboa mikono yangu na miguu yangu.
17Naweza kuhesabu mifupa yangu yote,
watu wananikodolea macho na kunisimanga.
18Wanagawana nguo zangu wao kwa wao,
na vazi langu wanalipigia kura.
19Lakini wewe, Ee Bwana,
usiwe mbali.
Ee Nguvu yangu,
uje haraka unisaidie.
20Okoa maisha yangu na upanga,
uhai wangu wa thamani kutoka nguvu za mbwa.
21Niokoe kutoka kinywani mwa simba,
niokoe kutoka pembe za mafahali mwitu.
22Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu,
katika kusanyiko nitakusifu wewe.
23Ninyi ambao mnamcha Bwana, msifuni!
Ninyi nyote wazao wote wa Yakobo, mheshimuni yeye!
Mcheni yeye, ninyi wazao wote wa Israeli!
24Kwa maana hakupuuza wala kudharau
mateso ya aliyeonewa;
hakumficha uso wake
bali alisikiliza kilio chake ili amsaidie.
25Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa,
nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wakuchao wewe.
26Maskini watakula na kushiba,
wale wamtafutao Bwana watamsifu:
mioyo yenu na iishi milele!
27Miisho yote ya dunia itakumbuka
na kumgeukia Bwana,
nazo jamaa zote za mataifa
watasujudu mbele zake,
28kwa maana ufalme ni wa Bwana
naye hutawala juu ya mataifa.
29Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu.
Wote waendao mavumbini
watapiga magoti mbele yake,
wote ambao hawawezi
kudumisha uhai wao.
30Wazao wa baadaye watamtumikia yeye;
vizazi vijavyo vitajulishwa habari za Bwana.
31Watatangaza haki yake kwa watu
ambao hawajazaliwa bado,
kwa maana yeye ametenda hili.
Copyright information for
SwhNeno