‏ Psalms 28

Kuomba Msaada

Zaburi ya Daudi.

1Ninakuita wewe, Ee Bwana, Mwamba wangu;
usiwe kwangu kama kiziwi.
Kwa sababu ukinyamaza
nitafanana na walioshuka shimoni.
2Sikia kilio changu unihurumie
ninapokuita kwa ajili ya msaada,
niinuapo mikono yangu kuelekea
Patakatifu pa Patakatifu pako.

3Usiniburute pamoja na waovu,
pamoja na hao watendao mabaya,
ambao huzungumza na jirani zao maneno mazuri,
lakini mioyoni mwao wameficha chuki.
4Walipe sawasawa na matendo yao,
sawasawa na matendo yao maovu;
walipe sawasawa na kazi za mikono yao,
uwalipe wanavyostahili.
5Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Bwana,
na yale ambayo mikono yake imetenda,
atawabomoa na kamwe
hatawajenga tena.

6 Bwana asifiwe,
kwa maana amesikia kilio changu
nikimwomba anihurumie.
7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,
moyo wangu umemtumaini yeye,
nami nimesaidiwa.
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha
nami nitamshukuru kwa wimbo.

8 Bwana ni nguvu ya watu wake,
ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
9Waokoe watu wako na uubariki urithi wako;
uwe mchungaji wao na uwabebe milele.
Copyright information for SwhNeno