‏ Psalms 36

Uovu Wa Mwanadamu

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Bwana.

1Kuna neno moyoni mwangu
kuhusu hali ya dhambi ya mwovu.
Hakuna hofu ya Mungu
mbele ya macho yake.
2Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno
hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake.
3Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu,
ameacha kuwa mwenye hekima na kutenda mema.
4Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya,
hujitia katika njia ya dhambi
na hakatai lililo baya.

5Upendo wako, Ee Bwana, unafika hadi mbinguni,
uaminifu wako hadi kwenye anga.
6Haki yako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama kilindi kikuu.
Ee Bwana, wewe huwahifadhi
mwanadamu na mnyama.
7Upendo wako usiokoma
ni wa thamani mno!
Watu wakuu na wadogo
hujificha uvulini wa mbawa zako.
8Wanajifurahisha katika wingi nyumbani mwako,
nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.
9Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima,
katika nuru yako twaona nuru.

10Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe,
haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.
11Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu,
wala mkono wa mwovu usinifukuze.
12Angalia jinsi watenda mabaya walivyoanguka:
wametupwa chini, hawawezi kuinuka!
Copyright information for SwhNeno