Psalms 38
Maombi Ya Mtu Anayeteseka
Zaburi ya Daudi. Maombi. 1Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako,wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.
2Kwa kuwa mishale yako imenichoma,
na mkono wako umenishukia.
3Hakuna afya mwilini mwangu
kwa sababu ya ghadhabu yako,
mifupa yangu haina uzima
kwa sababu ya dhambi zangu.
4Maovu yangu yamenifunika
kama mzigo usiochukulika.
5Majeraha yangu yameoza na yananuka,
kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
6Nimeinamishwa chini na kushushwa sana,
mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
7Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo,
hakuna afya mwilini mwangu.
8Nimedhoofika na kupondwa kabisa,
nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.
9Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku
yako wazi mbele zako,
kutamani kwangu sana
hakufichiki mbele zako.
10Moyo wangu unapigapiga,
nguvu zangu zimeniishia;
hata macho yangu yametiwa giza.
11Rafiki na wenzangu wananikwepa
kwa sababu ya majeraha yangu;
majirani zangu wanakaa mbali nami.
12Wale wanaotafuta uhai wangu
wanatega mitego yao,
wale ambao wangetaka kunidhuru
huongea juu ya maangamizi yangu;
hufanya shauri la hila mchana kutwa.
13Mimi ni kama mtu kiziwi, asiyeweza kusikia,
ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake,
14nimekuwa kama mtu asiyesikia,
ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.
15Ee Bwana, ninakungojea wewe,
Ee Bwana Mungu wangu, utajibu.
16Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie,
wala wasijitukuze juu yangu
mguu wangu unapoteleza.”
17Kwa maana ninakaribia kuanguka,
na maumivu yangu yananiandama siku zote.
18Naungama uovu wangu,
ninataabishwa na dhambi yangu.
19Wengi ni wale ambao ni adui zangu hodari,
wale wanaonichukia bila sababu ni wengi.
20Wanaolipa maovu kwa wema wangu
hunisingizia ninapofuata lililo jema.
21Ee Bwana, usiniache,
usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.
22Ee Bwana Mwokozi wangu,
uje upesi kunisaidia.
Copyright information for
SwhNeno