‏ Psalms 4

Sala Ya Jioni Ya Kuomba Msaada

Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi.

1Nijibu nikuitapo,
Ee Mungu wangu mwenye haki!
Nipumzishe katika shida zangu;
nirehemu, usikie ombi langu.

2Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu
kuwa aibu mpaka lini?
Mtapenda udanganyifu
na kufuata miungu ya uongo mpaka lini?
3Fahamuni hakika kwamba Bwana amewatenga
wale wamchao kwa ajili yake;
Bwana atanisikia nimwitapo.

4Katika hasira yako, usitende dhambi.
Mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya
mkiichunguza mioyo yenu.
5Toeni dhabihu zilizo haki;
mtegemeeni Bwana.

6Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye
kutuonyesha jema lolote?”
Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako.
7Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa
kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi.
8Nitajilaza chini na kulala kwa amani,
kwa kuwa wewe peke yako, Ee Bwana,
waniwezesha kukaa kwa salama.
Copyright information for SwhNeno