Psalms 56
Kumtumaini Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi. 1Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.
2Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,
wengi wananishambulia kwa kiburi chao.
3Wakati ninapoogopa,
nitakutumaini wewe.
4Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.
Mwanadamu apatikanaye na kufa,
atanitenda nini?
5Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu,
siku zote wanapanga shauri la kunidhuru.
6Wananifanyia hila, wanajificha,
wanatazama hatua zangu,
wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.
7Wasiepuke kwa vyovyote,
Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa.
8Andika maombolezo yangu,
orodhesha machozi yangu katika gombo lako:
je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?
9Ndipo adui zangu watarudi nyuma
ninapoita msaada.
Kwa hili nitajua kwamba Mungu
yuko upande wangu.
10Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Bwana, ambaye neno lake ninalisifu,
11katika Mungu ninatumaini, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
12Ee Mungu, nina nadhiri kwako,
nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.
13Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti
na miguu yangu kwenye kujikwaa,
ili niweze kuenenda mbele za Mungu
katika nuru ya uzima.
Copyright information for
SwhNeno