Psalms 59
Kuomba Ulinzi Wa Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Wakati Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue. 1Ee Mungu, uniokoe na adui zangu,unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.
2Uniponye na watu watendao mabaya,
uniokoe kutokana na wamwagao damu.
3Tazama wanavyonivizia!
Watu wakali wananifanyia hila,
ingawa Ee Bwana, mimi sijakosea
wala kutenda dhambi.
4Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia.
Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!
5Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli!
Zinduka uyaadhibu mataifa yote,
usionyeshe huruma kwa wasaliti.
6Hurudi wakati wa jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
7Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao,
hutema upanga kutoka midomo yao,
nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”
8Lakini wewe, Bwana, uwacheke;
unayadharau mataifa hayo yote.
9Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe,
wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
10Mungu wangu unipendaye.
Mungu atanitangulia,
naye atanifanya niwachekelee
wale wanaonisingizia.
11Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu,
au sivyo watu wangu watasahau.
Katika uwezo wako wafanye watangetange
na uwashushe chini.
12Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao,
kwa ajili ya maneno ya midomo yao,
waache wanaswe katika kiburi chao.
Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,
13wateketeze katika ghadhabu,
wateketeze hadi wasiwepo tena.
Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia
kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo.
14Hurudi jioni,
wakibweka kama mbwa,
wakiuzurura mji.
15Wanatangatanga wakitafuta chakula,
wasipotosheka hubweka kama mbwa.
16Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,
asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;
kwa maana wewe ndiwe ngome yangu
na kimbilio langu wakati wa shida.
17Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.
Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
Mungu unipendaye.
Copyright information for
SwhNeno