‏ Psalms 99

Mungu Mfalme Mkuu

1 Bwana anatawala,
mataifa na yatetemeke;
anakalia kiti cha enzi katikati ya makerubi,
dunia na itikisike.
2 Bwana ni mkuu katika Sayuni;
ametukuzwa juu ya mataifa yote.
3Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa:
yeye ni mtakatifu!

4Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki,
wewe umethibitisha adili;
katika Yakobo umefanya
yaliyo haki na sawa.
5Mtukuzeni Bwana Mungu wetu,
na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake;
yeye ni mtakatifu.

6Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake,
Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake;
walimwita Bwana,
naye aliwajibu.
7Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu;
walizishika sheria zake na amri alizowapa.

8Ee Bwana, wetu,
ndiwe uliyewajibu,
kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe,
ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.
9Mtukuzeni Bwana Mungu wetu,
mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu,
kwa maana Bwana Mungu wetu ni mtakatifu.
Copyright information for SwhNeno