‏ Song of Solomon 1

1Wimbo ulio bora wa Solomoni.

Shairi La Kwanza

Mpendwa 2Unibusu kwa busu la kinywa chako,
kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai.
3Manukato yako yananukia vizuri,
jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa.
Ndiyo sababu wanawali wanakupenda!
4Nichukue twende nawe, na tufanye haraka!
Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake.
Marafiki Tunakushangilia na kukufurahia,
tutasifu upendo wako zaidi kuliko divai.
Mpendwa Tazama jinsi ilivyo bora wakupende!
5Mimi ni mweusi, lakini napendeza,
enyi binti za Yerusalemu,
mweusi kama mahema ya Kedari,
kama mapazia ya hema la Solomoni.
6Usinikazie macho kwa sababu mimi ni mweusi,
kwa sababu nimefanywa mweusi na jua.
Wana wa mama yangu walinikasirikia
na kunifanya niwe mtunza mashamba ya mizabibu.
Shamba langu mwenyewe la mizabibu nimeliacha.
7Niambie, wewe ambaye ninakupenda,
unalisha wapi kundi lako la kondoo
na ni wapi unapowapumzisha kondoo wako adhuhuri.
Kwa nini niwe kama mwanamke aliyefunikwa shela
karibu na makundi ya rafiki zako?
Marafiki 8Kama hujui, ewe mwanamke mzuri kuliko wote,
fuata nyayo za kondoo,
na kulisha wana-mbuzi wako
karibu na hema za wachungaji.
Mpenzi 9Mpenzi wangu, ninakufananisha na farasi jike
aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao.
10Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli,
shingo yako ikiwa na mikufu ya vito.
11Tutakufanyia vipuli vya dhahabu,
vyenye kupambwa kwa fedha.
Mpendwa 12Wakati mfalme alipokuwa mezani pake,
manukato yangu yalisambaza harufu yake nzuri.
13Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane
kati ya matiti yangu.
14Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina
kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi.
Mpenzi 15Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Tazama jinsi ulivyo mzuri!
Macho yako ni kama ya hua.
Mpendwa 16Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Ee, tazama jinsi unavyopendeza!
Na kitanda chetu ni cha majani mazuri.
Mpenzi 17Nguzo za nyumba yetu ni mierezi,
na mapao yetu ni miberoshi.
Copyright information for SwhNeno